Na Benedict Liwenga, MAELEZO, Dodoma.
Wizara ya
Maliasili na Utalii imetoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua
tahadhari katika maeneo hatarishi hususan ambayo yamebainika kuwa na
Mamba au Viboko na kuwasilisha taarifa za matukio haraka kwa Viongozi wa
Vijiji husika na Maafisa Wanyamapori walio karibu ili kumbukumbu za
matukio na hatua stahiki ziweze kuchukuliwa mapema.
Kauli hiyo
imetolewa leo Bungeni Dodoma na Naibu Waziri, Wizara ya Maliasili na
Utalii, Mhe. Ramo Makani wakati akijibu swali la Mbunge wa Bunda Mjini,
Mhe. Esta Bulaya ambaye alitaka kujua jinsi gani Serikali imejipanga
katika kuokoa maisha ya Wananchi kutokana na hatari kubwa ya mamba hao.
Mhe. Makani
amesema kwamba baadhi ya Vijiji vilivyotajwa na Mhe. Mbunge Esta Bulaya
vinapatikana na Ziwa Viktoria na mazingira hayo yanasababisha kuwepo na
mwingiliano wa shughuli za kibinadamu na makazi ya wanyamapori kama vile
mamba pamoja na viboko ambayo yanaweza kusababisha matukio ya wananchi
kuuawa na kujeruhiwa na wanayamapori hao.
"Wizara
yangu imepokea taarifa zilizowasilishwa na Halmashauri ya Wilaya ya
Bunda ambazo zinaendelea kuhakikiwa, kwamba katika kijiji cha Guta jumla
ya wananchi wanne waliuawa na wengine tisa kujeruhiwa na mamba katika
kipindi cha mwaka 2013 hadi 2015", alisema Mhe. Makani.
Aliendelea
kusema kwamba katika kipindi hicho, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na
kupokelewa kuhusu matukio katika vijiji vya Tairo, Nyamtwali na Njabeu.
Alifafanua
kuwa, Kifungu cha 69 cha Sheria ya Kuhifafhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka
2009, kimempa mamlaka Mkurugenzi wa Wanyamapori kukasimu majukumu ya
kushughulikia masuala ya Wanyamapori wakali na waharibifu kwa Afisa
aliyeidhinishwa.
Aidha,
Sheria imeainisha utaratibu wa kutoa taarifa za matukio kuanzia kwa
Mtendaji wa kijiji, Maafisa Wanyamapori walioko karibu hadi Wizarani kwa
hatua zaidi.
"Ili kuokoa
maisha ya wananchi kutokana na hatari ya mamba na viboko katika vijiji
vilivyotajwa, Wizara yangu kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori
(TAWIRI) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda itafanya
tathmini ya ongezeko la mamba, na iwapo itadhihirika kuwa idai yao ni
kubwa kuliko viwango vinavyokubalika hatua stahiki zitachukuliwa ikiwa
ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuwavuna wanyama hao", alisema Mhe.
Makani.
Aliongeza
kuwa utaratibu huo utatumika katika maeneo yote yenye uhatarishi wa
mamba na viboko. Wizara itaendelea kutoa elimu kuhusu uhifadhi, jinsi ya
kujilinda na kujiepusha na wanayamapori wakali na waharibifu wakiwemo
mamba pamoja na taratibu za kuwasilisha madai ya malipo ya kifuta jasho
na machozi kwa wale watakaoathirika.
"Pamoja na
jitihada hizo za Serikali, Wizara inatoa wito kwa wananchi kuendelea
kuchukua tahadahari katika maeneo hatarishi hususan ambayo yamebainika
kuwa na Mamba au Viboko na kuwasilisha taarifa za matukio hayo haraka
kwa Viongozi wa Vijiji husika na Maafisa Wanyamapori", alisisitiza Mhe.
Makani.
0 comments:
Post a Comment