Home » » Waziri Ndalichako ang’ara bungeni

Waziri Ndalichako ang’ara bungeni

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako
BAJETI ya Wizara ya Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi, juzi ilipitishwa kwa namna ya kipekee tofauti na ilivyozoeleka.
Hali hiyo inatokana na wabunge wa vyama vyote, kuungana na kumtetea Waziri wake, Profesa Joyce Ndalichako, wakitaka apewe muda aboreshe elimu.
Wabunge wamepitisha bajeti ya Sh trilioni 1.3 huku wakisisitiza serikali iboreshe elimu nchini, ikiwa ni pamoja na kuondoa changamoto mbalimbali.
Wakati Bunge likiwa limekaa kama kamati, ambako wabunge hushika mshahara wa waziri hadi wapate majibu ya kuridhisha, kwa upande wa wizara hii, waziri husika alitetewa na baadhi ya wabunge wakiwemo wa upinzani.
Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi ) alilalamikia tatizo la vitabu shuleni, ikiwemo kukosewa kwa mitaala, jambo alilotaka waziri kuzungumzia.
Akijibu suala hilo, Ndalichako alisema nyaraka alizonazo mbunge yeye hana, hivyo aliomba kupatiwa afanyie kazi, lakini Mbatia alikataa na kusema nyaraka hizo si za siri, kwani zipo kwenye mitandao ya elimu huku kukiwa na vitabu vinavyotumika shuleni.
Baada ya mjadala wa muda mrefu, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Maendeleo) aliingilia suala hilo na kusema matatizo ya mitaala ni mapana.
Alishauri suala hilo lirudishwe kwenye Kamati ya Bunge inayoshughulikia suala hilo kwa ajili ya kufanyiwa kazi. Mbatia alikubaliana na ushauri wa Zitto na kurejesha shilingi, kisha kuendelea na mjadala mwingine.
Awali, alipoanza kujibu hoja mbalimbali za wabunge, Profesa Ndalichako aliwashukuru wabunge wote bila kujali tofauti za kisiasa, kwa ushauri mbalimbali waliotoa na kusema atahakikisha anafanyia kazi.
Waziri huyo aliyeteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mbunge na kisha kupewa uwaziri, ikiwa ni mara yake ya kwanza kusoma hotuba ya wizara hiyo, alikuwa akishangiliwa mara kwa mara na wabunge wa chama tawala na upinzani.
Ilipofika wakati wa kuwahoji wabunge, Mwenyekiti wa Bunge, Musa Zungu alipohoji wanaoafiki waseme ‘Ndiyo’, Bunge lote liliitikia. Hakuna aliyesema ‘Hapana’.
Aidha Bunge lilizizima kwa makofi kutoka kwa wabunge wote kwa dakika kadhaa, kabla ya kuahirishwa huku kwa umoja wao wakielekea katika kiti alichokaa Waziri Ndalichako kumpongeza. Pia kwenye majadiliano, yapo baadhi ya maeneo ambayo wabunge kwa pamoja, walikubaliana kumpa muda waziri kufanyia kazi.
Akizungumzia mabadiliko ya mara kwa mara ya mitaala na mifumo mingine ya elimu, Ndalichako alisema katika kuboresha elimu, lazima kuwe na mabadiliko. Alisema katika utawala wake, watafanya mabadiliko kwa kushirikisha wadau wa elimu.
Aliomba jamii kumuunga mkono, pale wanapofanya mabadiliko. “Wabunge wengi mmechangia kwa uchungu kuhusu ubovu wa elimu nchini, hivyo tumeanza kufanyia marekebisho ili kuboresha elimu; hivyo ni vema kutuunga mkono,” alisema.
Chanzo Kutoka Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa