Home » » Askari 1,657 Wapandishwa Vyeo kwa Mwaka wa Fedha 2014/15

Askari 1,657 Wapandishwa Vyeo kwa Mwaka wa Fedha 2014/15

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Jonas Kamaleki

Maelezo

Dodoma
 
Serikali imewapandisha vyeo  askari polisi 1,657 wa  vyeo vya uongozi mdogo kwa mwaka wa fedha 2014/2015 kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.

Akijibu swali la mbunge wa Kojani, Mhe. Hamad Salim Maalim kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Naibu waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi , Mhe. William Ole Nasha  amesema askari hupanda vyeo kama ilivyo kwa watumishi wengine wa umma na vyeo hivi huambatana na kuongezeka kwa maslahi yao kulingana na cheo alichopandishwa.

Ole Nasha amekiri kuwepo kwa ucheleweshwaji wa ulipaji wa mishahara inayolingana na vyeo katika jeshi la polisi na kufafanua kuwa yapo matatizo ya kiufundi yanayojitokeza wakati wa zoezi la kurekebisha mishahara ambayo husababisha baadhi ya askari kutorekebishiwa mishahara yao.

Aliongeza kuwa  juhudi hufanyika ili kutatua tatizo hilo mara mhusika anapowasilisha malalamiko yake Makao Makuu ya Jeshi hilo.

Naibu Waziri huyo alisema Kitengo cha Maslahi Polisi Makao Makuu hupokea malalamiko yao na kuwasiliana na Mamlaka za ulipaji ili kutatua tatizo husika.

Ole Nasha ametoa wito kwa skari yeyote ambaye amepatwa na tatizo kama hilo  awasiliane na viongozi katika Kamandi yake au Makao Makuu ya Polisi Idara ya Maslahi ili kupata ufumbuzi wa tatizo hili haraka iwezekavyo.

Kuhusu suala la ucheleweshwaji mishahara kuchangia katika vitendo vya polisi kujihusisha na rushwa, Ole Nasha alisema hilo suala halipo kwani polisi wanafanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi na kwamba malalamiko ya ucheleweshwaji yanapotokea hushughulikiwa.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa