NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Selemani Jafo amewanyooshea kidole wakuu wa mikoa nchini
wanaosuasua katika agizo la rais la kuhakikisha kila shule ya msingi na
sekondari, inakuwa na madawati ifikapo mwisho wa mwezi huu.
Alisema hayo jana wakati akifungua majengo mapya matatu ya Shule ya
Msingi Nzuguni B katika Manispaa ya Dodoma, ambayo yamejengwa kwa nguvu
za wananchi na wadau. Jaffo alisema katika maeneo mengi, kazi ya
utengenezaji madawati inakwenda vizuri kwani katika mikoa mingi hali
inaonesha kazi hiyo inakwenda vizuri.
“Wakuu wa mikoa wanaosuasua watapimwa kwa kigezo hicho katika
utendaji kazi wao,” alisema Naibu Waziri. Alisema baada ya Juni 30,
ambayo ndiyo siku iliyowekwa katika kuhakikisha kila shule inakuwa na
madawati, itafanyika tathimini nchi nzima kuona kama kazi hiyo
imefanikiwa.
“Niwatie moyo wakuu wa mikoa kazi yao ni nzuri na waendelee kujipanga
katika kuhakikisha wanatimiza kazi hii,” alisema na kuongeza kuwa
Aprili alifanya ziara katika shule hiyo na kukuta ikiwa na changamoto
nyingi ikiwemo uhaba wa vyumba vya madarasa huku wanafunzi wakiwa
wamekaa chini kutokana na uhaba wa madawati.
Pia katika shule hiyo kulikuwa na vyumba vitatu vya madarasa ambavyo
vilikuwa havijakamilika ndipo alipoagiza kukamilishwa kwa majengo hayo
na wanafunzi kupatiwa madawati. Alisema agizo hilo limetekelezwa
kikamilifu na majengo hayo yamekamilika huku madawati 264 kati ya 400
tayari yamepelekwa shuleni hapo na wanafunzi wanakalia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma, Azimina Mbilinyi alisema
changamoto kubwa iliyokuwepo katika shule hiyo ilikuwa uhaba wa
madawati, ambayo awali kulikuwa na madawati 84 kati ya 568
yaliyohitajika.
Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde alisema ataendelea kuunga
mkono juhudi za maendeleo. Mavunde ambaye pia ni Naibu Waziri, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Ajira, Kazi na Vijana alitoa Sh 300,000 ili huduma ya maji
irudishwe huku akiahidi kusaidia kompyuta.
Chanzo Gazeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment