Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Katika kuthibiti matumizi ya
magari yanayoingia Nchini kwa msamaha wa kodi Serikali imesema kuanzia
Julai Mosi magari hayo sasa yatakuwa na namba na rangi maalum.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango alipokuwa akiongea na waandishi wa
habari mjini Dodoma kuhusu tamko la kuondoa misamaha ya kodi kwenye
taasisi za dini kwa kuwa zinatoa huduma za kijamii kama shule na
hospitali.
“Kwa kutambuua mchango mkubwa wa
Taasisi mbalimbali za kidini katika utoaji wa huduma za elimu na afya,
napendekeza kufuta utaratibu niliotangaza katika hotuba ya bajeti na
badala yake Serikali itaimarisha zaidi hatua mbalimbali za uthibiti
misamaha ya kodi ikiwemo magari yaliyoingia kwa msamaha wa kodi kuwa na
namba na rangi maalum,” alifafanua Mhe.Dkt. Mpango.
Aliendelea kutaja hatua nyingine
kuwa ni taasisi za kidini kuwasilisha vifaa vinavyotarajiwa kununuliwa
kutoka nje ya nchi kila mwazo mwa mwaka wa kalenda na kuthibitisha kama
vifaa vilivyopewa msamaha mwaka uliopita vilitumika kama sheria
inavyotaka.
Pia, kuwasilisha majina ya watu
walioidhinishwa na Shirika au Taasisi kuandika barua ya kuomba msamaha
wa kodi, wakiainisha cheo, saini, picha, anwani na namba zao za simu ili
kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania kufuatilia bidhaa zilizoombewa na
kupewa msamaha kama zimepata kibali cha taasisi hizo.
Vile vile taasisi hizo zinatakiwa
kupata barua kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Serikali ya Mtaa na Mkuu wa
Wilaya mahali Taasisi au Mradi unaotekelezwa ulipo.
Mhe. Mpango amesema kuwa hatua
hizo zimekuja kutokana na bidhaa zinazoombewa msamaha wa kodi kutumika
tofauti na kusudi la msamaha huo.
Aidha ametoa tahadhari kwa
mashirika ya kidini kuanzia sasa, kuhakikisha kuwa yanafuata taratibu
zote na Kuzingatia masharti ya msamaha unaotolewa ili kuepuka kufutiwa
leseni zao pale zitakapokwenda kinyume na sheria na kanuni zilizowekwa.
0 comments:
Post a Comment