Na Anna Nkinda - Dodoma
Serikali imewataka wanamichezo kujiepusha na matumizi ya dawa za
kuongeza nguvu mwilini au matumizi ya dawa zisiruhusiwa kwa wanamichezo
kwa kufanya hivyo wanaweza kupata madhara ya kiafya na kufungiwa kushiriki katika mashindano ya kitaifa na kimataifa.
Mwito huo umetolewa leo na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura wakati akifunga mashindano
ya michezo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vilivyopo mkoani Dodoma
yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri uliopo mkoani humo.
Mashindano
hayo yaliyojumusha wanafunzi kutoa vyuo vikuu vya Dodoma, Mipango, St.
John na Chuo cha Biashara (CBE) yaliandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Pensheni wa PSPF .
Mhe.
Wambura alisema kwa kipindi cha mwaka 2015/16 wanamichezo 14
walichukuliwa vipimo vyao na kupelekwa katika maabara za Kimataifa na
wote kukutwa salama na hivyo kuwapongeza wanamichezo hao ambao wameweza kujilinda kwa kutotumia dawa hizo.
Alisema, “Viongozi wote wa Vyama vya Michezo, waalimu na madaktari wa wanamichezo tuungane kwa pamoja kupiga vita matumizi ya dawa za kuongeza nguvu michezoni. Msisite kuchukua hatua kali pale inapothibitika bila shaka yeyote kuwa mwanamichezo ametumia dawa za kuongeza nguvu mwilini”.
Mhe.
Naibu Waziri pia aliwasisitiza wanafunzi wa vyuo vyote nchini kushiriki
katika michezo na kusoma kwa bidii ili waweze kujikwamua kiuchumi na
kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.
“Vijana wakitumia muda wao wa ziada kushiriki katika Michezo watajiepusha na mazingira hatarishi yatakayowapelekea
kuwa wazurulaji, kupata maambukizi ya VVU, kutumia dawa za kulevya na
kushiriki katika vitendo vya uhalifu”, alisisitiza Mhe. Wambura.
Aidha
Mhe. Naibu Waziri huyo aliwakumbusha Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa
PSPF waendelee kudhamini michezo kama hiyo ili kuweza kuhamasisha vijana
kushiriki katika michezo kwani Michezo ni ajira, afya na inaimarisha
umoja.
Mhe. Naibu Waziri alisema, “Napenda
kuwahakikishia mkifanya hayo hakika mtaendelea kuwa Mfuko wa chaguo la
kwanza kwa wanachama wapya kama ilivyo hivi sasa, kwani hawa wanafunzi
ndio wanachama wa baadae haswa ikizingatiwa hivi sasa kinachovutia
wanachama wapya ni huduma bora na kuwajali wateja wenu”.
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi wa PSPF wa Mkoa
wa Dodoma Salim Kimbute aliwaomba wanafunzi walioshiriki katika
mashindano hayo kufikisha elimu kwa jamii hususani vijana ambao
wameajiriwa au wanaotarajiwa kuajiriwa hivi karibuni katika maeneo
mbalimbali ili nao waweze kufurahia maisha bora ya sasa na baadaye kwa
kujiunga na PSPF.
“Katika
kuhakikisha PSPF inakuwa karibu na jamii, Mfuko unafadhili mashindano
kwa wanafunzi wa vyuo katika Mikoa mbalimbali ili kuweza kuwahamasisha
kushiriki katika michezo na vilevile kuwapa elimu ya hifadhi ya jamii
ili kuhakikisha kila Mtanzania anafaidika na Hifadhi ya Jamii”, alisema
Kimbute.
PSPF
iliandaa mashindano hayo ili kuweza kuhamasisha na kutoa fursa kwa
wanafunzi kujifunza umuhimu wa michezo na hifadhi ya jamii.
Washindi
wa kwanza katika mashindano hayo ambao walishiriki michezo ya mpira wa
pete, miguu, wavu na kikapu walipewa zawadi ya Kombe na vifaa vya
michezo, na washindi wengine walipewa zawadi za vifaa vya michezo.
0 comments:
Post a Comment