Home » » Wabunge, mameya watofautiana kodi za majengo

Wabunge, mameya watofautiana kodi za majengo

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

KUHAMISHWA kwa jukumu la ukusanyaji wa kodi za majengo kutoka katika halmashauri na kupelekwa katika Mamlaka ya Mapato (TRA), kumeungwa mkono na baadhi ya wabunge, jambo lililoonesha kwenda kinyume na maoni ya mameya wa halmashauri mbalimbali nchini.
Jana Mbunge wa Singida Mjini, Musa Sima (CCM), aliunga mkono hatua hiyo ya serikali na kusema anachoona ni serikali kupunguzia mzigo halmashauri za wilaya, miji na manispaa katika ukusanyaji wa kodi hiyo. Aliitaka serikali kama ilivyoahidi, kupeleka fedha zote watakazokusanya katika kodi hiyo katika halmashauri husika.
Sima aliungana na Mbunge wa Mkalama, Alan Kiula (CCM), ambaye juzi alisema TRA ina wafanyakazi wenye uzoefu na vitendea kazi vya kukusanya kodi kuliko halmashauri yoyote, hivyo ni sahihi wakabidhiwe jukumu hilo.
Kwa mujibu wa Kiula, halmashauri nyingi zilishindwa hata kukadiria majengo ili kupata kodi stahiki lakini kwa hatua hiyo ya serikali, anatarajia halmashauri sasa zitapata kodi stahiki.
Mbunge wa Chemba, Juma Nkhamia (CCM), alienda mbali zaidi na kutaka wakati wa kukusanya kodi hizo, watendaji hao wa TRA pia wahoji wahusika walikopata fedha za kujenga majumba makubwa. Pia aliitaka Serikali kuhakikisha kuwa ahadi ya kurejesha fedha hiyo, inatimizwa ili halmashauri zifanye kazi zake.
Katika hotuba ya Bajeti ya Serikali ya 2016/2017, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, alisema kodi za majengo hazitakusanywa na halmashauri, badala yake TRA ndiyo inayopewa mamlaka hayo ya kukadiria, kukusanya, kuhifadhi na kuiwakilisha katika halmashauri husika.
Mbali na TRA kupewa mamlaka ya kukusanya kodi ya majengo, serikali pia ilipendekeza kupunguza misamaha ya kodi za majengo, ili majengo mengi zaidi yaingizwe katika orodha ya kulipa kodi.
Chanzo Gazeti La Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa