Home » » Wizara ya Fedha na Mipango yatoa elimu ya ubia kwa wabunge

Wizara ya Fedha na Mipango yatoa elimu ya ubia kwa wabunge

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.Na: Lilian Lundo – Dodoma – Maelezo

Wizara ya Fedha na Mipango leo Mjini Dodoma imetoa semina Kuhusu  ubia kati ya Sekta Umma na Sekta  Binafsi kwa wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Semina hiyo iliyofunguliwa na Naibu Spika Mhe. Tulia Ackson  ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye semina hiyo ambapo  mada  kuhusu utaratibu  huo iliwasilishwa na Kamishna  anasimaia Idara inayoratibu  ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kutoka Wizara hiyo Dkt. Frank Mhilu.

“Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ni mkataba wa muda mrefu wa kuanzia miaka 5 hadi 30 na kuendelea kati ya kampuni ya mwekezaji binafsi na Taasisi ya Serikali ambapo mwekezaji binafsi anajenga miundombinu  au anapewa miundombinu ili aiboreshe kwa lengo la kutoa huduma ya umma kwa gharama nafuu  na baada ya mkataba kwisha miundombinu husika hurejeshwa kwa Serikali,” alifafanua Dkt. Mhilu.

Aidha Dkt. Mhilu aliendelea  kusema kuwa, ili kufanikiwa katika ubia lazima kuwe na maandalizi muhimu ambayo ni kuibua fursa za uwekezaji kwa mujibu wa mpango wa Taifa wa maendeleo, kufanya uchambuzi yakinifu ili kujiridhisha kuwa mradi una manufaa kwa uwekezaji kwa utaratibu wa ubia.

Vile vile kuandaa ardhi na miundombinu wezeshi, kutangaza miradi kwa uwazi, kujiridhisha ubora wa zabuni ya mwekezaji na namna ambavyo fedha zitapatikana na uwezo wa Taasisi ya Umma kusimamia mradi husika.

Pia Dkt. Mhilu aliitaja miradi ambayo iko katika hatua mbalimbali za ubia kuwa ni mradi wa mabasi ya haraka Dar es Salaam (DART), mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi III (TANESCO), mradi wa barabara ya tozo wa  Dar – chalinze (TANROADS), mradi wa uzalishaji wa madawa muhimu (MSD) pia iko miradi ambayo imechambuliwa na kutolewa taarifa zake kwa ajili ya kuboreshwa.

Dkt. Mhilu amesema kuwa utaratibu wa ubia sasa utakuwa kwenye ofisi moja ambayo ni Wizara ya Fedha na Mipango ili kuweka ufanisi katika utekelezaji wake ikiwa ni maamuzi ambayo yamefanyika katika awamu ya Tano ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Miradi ya ubia ni mkombozi katika kuboresha Bajeti ya Serikali na kuharakisha maendeleo endapo tu fursa za uwekezaji zitabuniwa vizuri, miradi itaandaliwa vizuri na taarifa sahihi zitatumika katika kuandaa miradi, wawekezaji wapatikane  kwa njia ya haki, uwazi na ushindani pamoja na mwekezaji kusimamiwa vyema katika ujenzi, uendeshaji na urejeshaji wa miundombinu.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa