Na RAMADHAN HASSAN, BAHI
MAJI ya kunywa ya chupa yamemtokea puani Mhandisi wa Maji wa Wilaya
ya Bahi mkoni Dodoma, Deus Mchele, alipojikuta katika wakati mgumu
baada ya kunywa maji hayo kwenye mkutano wa Kijiji cha Mchito.
Kitendo hicho kilizua vurugu kwa wanakijiji hao kuja juu wakisema mhandisi huyo wa maji ameonyesha dharau kwao.
Walisema hawajawahi kunywa hata maji ya bomba au kisima kisafi tangu kianzishwe kijiji hicho.
Tukio hilo lilitokea juzi katika kijijini hapo wakati Mhandisi
Mchele, alipokuwa ameongozana na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,
Benardetha Januari.
Wote kwa pamoja walijikuta wakiwashiwa moto na wananchi kutokana na tukio hilo.
Viongozi hao walikwenda katika kijiji hicho kuzungumza na wananchi
kuwaeleza sababu za kukwama mradi wa maji kijijini hapo kwa zaidi ya
miaka mine.
Katika kikao hicho, Mhandisi Mchele alikuwa amebeba chupa ya maji
safi ya Uhai na kila wakati alikuwa akiinyanyua na kunywa, hali
iliyoanza kuzua minong’ono ya chinichini kutoka kwa wananchi.
Dakika tano baada ya kufika viongozi hao, alisimama Mwenyekiti wa
Kijiji cha Mchito, Moses Daniel na kufungua mkutano huo kabla ya kumpa
fursa Diwani wa Kata wa hiyo, Mathew Malilo (CCM), ambaye moja kwa moja
aliruhusu maswali kutoka kwa wananchi.
Ilipotolewa fursa hiyo, alisimama mmoja wa wananchi wa kijiji hicho,
Ashery Mtonga ambaye ‘alimlipua’ mhandisi Mchele akidai kuwa alikuwa
ameonyesha dhararu kubwa kwao kwa kwenda na chupa ya maji wakati kijiji
hicho hakijawahi kuona maji ya bomba kwa zaidi ya miaka mitano.
“Nyie mnakuja na maji ya chupa watoto wetu je? Mradi wa maji katika
kijiji hiki una miaka minne hatujawahi kuona hata tone la maji… sisi
leo (juzi) tunataka mtuambie maji yataanza kutoka lini.
“Kila kukicha tunakunywa maji ya madimbwi ambayo nayo hukauka. Nyie
hapo mmekuja na maji ili tuwaone mnavyofaidi… jamani hii kweli ni haki?”
alihoji Mtonga.
Naye Jemima Soweya, alisema alishangazwa na mhandisi huyo kwenda na
maji huku wao wakiwa hawajui hatima yao na kila wakati hulazimika
kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo.
Mhandisi Mchele alipopewa nafasi ya kutoa ufafanuzi kuhusu mradi huo
wa maji, alisema wilaya ilitoa kazi ya utengenezaji wa mradi huo kwa
Kampuni ya Intersystem Holding Company Ltd mwaka 2012.
Alisema hadi sasa imeshindwa kukamilisha kwa mujibu wa mkataba wa makubaliano.
Kutokana na hali hiyo ilibainika mkandarasi huyo wa mradi wa maji
alishindwa kuutekeleza kwa wakati hivyo ikaamuriwa afukuzwe na yeye
akawasilisha makakamiko ya kutaka alipwe Sh milioni 100.
“Baada ya kuleta malalamiko tukaona hatuwezi kumpa mkataba mtu mwingine mpaka tujadiliane tupate majibu ya mgogoro huu.
“Ila kwa kweli mkandarasi yule hakuwa na uwezo wa kujenga mradi huu.
Na mradi huu ulikuwa unatekelezwa kwa gharama ya Sh milioni 246 na
tayari tulikuwa tumeshamlipa robo tatu ya fedha,” alisema.
Mchele alisema hajalala kwa vizuri miaka minne sababu ikiwa ni mradi huo wa maji wa Mchito kutokukamilika.
Maelezo hayo yaliamsha hasira kwa wananchi na akasimama mwananchi
mmoja, Anderson Ndelele aliyehoji kama mhandisi huyo wa wilaya
hajalala kwa miaka minne angekuwa hai mpaka sasa?
“Leo mngeona aibu hata kuja na hayo maji ya chupa tena unatuambia
hujalala kwa muda wa miaka minne ungekuwa hai kweli si unatudanganya!
“Nyie endeleeni na kesi yenu sisi tunataka maji leo (juzi)…
hamuondoki mpaka tupate maji, semeni maji yatatoka lini hapa
Mchito,’’alisisitiza Ndelele,
Alipotakiwa kutoa majibu ya maswali hayo, Mhandisi Mchele aligoma
akisema hakuwa na majibu hali iliyomlazimu diwani Malilo kuwatuliza
wananchi hao.
Chanzo na Mwananchi
0 comments:
Post a Comment