POLISI mkoani Dodoma imetoa onyo kwa watu watakaojaribu kuvuruga
mkutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaotarajiwa kufanyika Julai 23,
mwaka huu .
Aidha, imeonya wakazi wa mjini hapa watakaobainika kuhifadhi watu
wanaodhamiria kufanya vurugu kwenye mkutano huo kuwa pia watachukuliwa
hatua.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema watuhumiwa wanne waliokamatwa juzi
ambao ni viongozi wa Baraza la Vijana (Bavicha) watafikishwa mahakamani
leo kujibu tuhuma zinazowakabili.
Watuhumiwa hao na vyeo vyao kwenye Bavicha ni Patrobas Katambi
(Mwenyekiti- Taifa), Julius Mwita (Katibu Taifa) na George Tito ambaye
ni mwenyekiti wa baraza hilo mkoa wa Mbeya.
Mwingine aliyekamatwa ni mratibu wa uenezi na uhamasishaji wa baraza
hilo, Edward Simbeye. Wote walikamatwa kwa tuhuma za kuhamasisha kashfa
dhidi ya serikali.
Alitoa onyo hilo wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari na
maofisa mbalimbali wa polisi wa mkoani juu ya kile alichoeleza, jaribio
la kuleta vurugu katika mkutano huo wa CCM.
‘’ Jeshi halitawaacha bali hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo
kuwachukulia hatua za kisheria kwa wale wenye nyumba binafsi ambao
watawahifadhi wenye nia mbaya na mkutano wa CCM,’’alisema.
Alisema kumekuwa na viashiria vya kutokea vurugu katika mkutano huo
na kusema polisi imejipanga kukabiliana na watakaohusika kusababisha
hali hiyo.
“Tutahakikisha mkutano huo unakuwa ni wa amani na ole wako ulete
vurugu katika mkutano huo, watafanya wale ambao utawahusu tu,’’alisema.
Kwa mujibu wa kamanda, wanaoshikiliwa walikamatwa wakiwa katika
harakati za kuhamasisha wengine kuichukia serikali kwa kauli na mavazi
yenye kubeba ujumbe wa uchochezi.
Mambosasa alisema kuwa polisi tayari wana taarifa kuwa watu hao
wamepanga kufikia kwenye nyumba za watu binafsi badala za kulala kwenye
nyumba za wageni, hivyo alidai wale wote watakaobainika kuwahifadhi
watakamatwa na kufunguliwa mashtaka kutokana na kosa la kuwatunza
watuhumiwa hao.
Alisisitiza kuwa polisi haiko tayari kuona makundi hayo ya kisiasa
yakivuruga amani na utulivu uliopo ndani ya mkoa huo wa Dodoma kwa
kisingizio cha siasa na endapo yatajitokeza yatakutana na mkono wa
sheria.
Chanzo Na Gazeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment