Home » » Wanne wa familia moja wafa moto

Wanne wa familia moja wafa moto

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Lazaro Mambosasa
HUZUNI imetanda katika wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, baada ya ajali ya moto wa kibatari kuteketeza watoto wanne wa mama mmoja, waliokuwa wamefungiwa chumbani na dada anayewalea.
Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana katika mtaa wa Nyerere, mji mdogo wa Kibaigwa wilayani Kongwa, wakati mama wa watoto hao aliposafiri kwenda shambani Kiteto mkoani Manyara, kwa ajili ya kuvuna mazao na kuwaacha watoto wake mikononi mwa dada, aliyekuwa akimsaidia kuwalea.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema chanzo cha ajali hiyo ni mlipuko wa kibatari kilichokuwa ndani ya chumba walicholala watoto hao, ambacho kilichoma godoro na kuteketeza nyumba yote.
Moto huo ulioanzia katika chumba hicho, umeelezwa kuteketeza nyumba yote ya vyumba sita iliyojengwa kwa tofali za udongo mali ya Nelson Mdachi.
Kamanda Mambosasa aliwataja watoto hao kuwa ni Elizabeth Nelson (11) mwanafunzi wa darasa la saba, Samweli Mdachi (7) anayesoma darasa la kwanza na Nase Mgomba (9) anayesoma darasa la pili katika shule ya msingi Miembeni na Peter Lema (9) mwanafunzi darasa la tatu shule ya msingi St Paulo.
Kutokana na ajali hiyo, Kamanda Mambosasa amewakumbusha wazazi wasiache watoto peke yao nyumbani kwa kuwa ni hatari kwani ajali ikitokea ni vigumu kuokolewa.
Taarifa kutoka kwa watu wa karibu na majirani wa familia hiyo, zimedai kuwa mama wa familia hiyo alikwenda shambani kuvuna mazao katika wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara na kuwaacha watoto hao chini ya uangalizi wa msichana aliyefahamika kwa jina moja la Ester.
Kwa mujibu wa madai yao, ilipofika usiku Ester anayetajwa kuwa na jukumu la kulea watoto hao, alitoka na kwenda kusikojulikana huku akiwafungia watoto hao kwa nje.
Mkazi wa Kibaigwa, Denis Luhunga, alipozungumza na gazeti hili kuhusu ajali hiyo alidai kuwa kibatari kilipolipuka, kilisababisha godoro kushika moto na kuteketea kwa watoto hao. “Aliwafungia watoto ndani akaacha kibatari kinawaka, baada ya kulipuka moshi mwingi ulijaa ndani,” alidai Luhunga.
Kuhusu alipo baba wa familia hiyo, mkazi mwingine wa eneo la tukio hilo, Paulo Sauli alisema baba wa watoto hao, aliyemtaja kwa jina la Nelson Mdachi, alishakufa miaka mitatu iliyopita na jukumu la kuwalea aliachiwa mama yao.
Alifafanua kuwa baba huyo ambaye wakati wa uhai wake alifahamika kwa jina maarufu la ‘Moja kwa moja’, alikufa baada ya kuanguka kutoka juu ya mti alipokuwa akirina asali na tangu hapo, jukumu la kulea likabaki kwa mama mzazi wa watoto hao.
“Tukio hilo limetusikitisha sana ni tukio baya maana wameteketea kabisa hajulikani nani ni nani,” alisema Sauli na kuongeza, “Hata Ester hafahamiki alipo, kuna watu wengi lakini tumemuangalia hapa msibani hatumuoni.”
Taarifa nyingine kutoka eneo la tukio, zilidai kuwa Mdachi alizaa na mama huyo watoto wawili na baada ya kufariki, mama huyo alizaa watoto wengine wawili na wanaume wengine.
Ajali barabarani Katika tukio lingine, ajali nyingine imetokea eneo la mlima Sekenke wilayani Iramba kwenye barabara kuu ya Singida – Nzega na kusababisha vifo vya watu wanne papo hapo na majeruhi wawili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni dereva wa gari hilo Thabit Ally na abiria, Christopher Kilindiro (30) na Rajabu Shabani (25) ambao ni wafanyabiashara na wakazi wa Igunga mkoani Tabora na mwanamume mmoja ambaye jina lake halijapatikana.
Kwa mujibu wa Sedoyeka, waliojeruhiwa ni Lausius Charles Haule (15) mwanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Igunga na Marwa Charles (37) mfanyabiashara na mkazi wa Igunga na wamelazwa katika hospitali ya Kiomboi wilayani Iramba kwa matibabu.
Kamanda Sedoyeka amesema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi majira ya saa 3.00 asubuhi katika kijiji cha Misigiri na kuhusisha gari la mizigo lenye usajili namba T.716 MMI na trela T. 391 DCY aina ya Scania mali ya Hascam Investment & General Supplies Ltd ya jijini Dar es Salaam.
Alisema gari hiyo likisafiri kutoka Moshi kwenda Mwanza, huku likiwa limepakia shehena ya mbolea liliacha njia na kutumbukia darajani na kusababisha vifo vya watu hao wanne na majeruhi wawili.
Alisema uchunguzi wa awali wa chanzo cha ajali hiyo, umebaini kuwa breki za gari hilo zilishindwa kufanya kazi yake ipasavyo.
Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma na Abby Nkungu, Singida.
Chanzo Na Habari leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa