Home » » Watanzania waaswa kudumisha amani iliyopo nchini.

Watanzania waaswa kudumisha amani iliyopo nchini.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiongea leo na wakazi wa Dodoma na watanzania kwa ujumla wakati wa shughuli ya maadhimisho ya Siku ya kumbukumbu ya Mashujaa Tanzania na kuwaasa watanzania kudumisha amani ambayo ilipatikana baada ya Mashujaa wetu kuipigania na hata kujitoa uhai wao kwa ajili ya Taifa.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili  Mheshimiwa Alhaji Ali Hassan Mwinyi akiongea leo na wakazi wa Dodoma na watanzania kwa ujumla wakati wa shughuli ya maadhimisho ya Siku ya kumbukumbu ya Mashujaa Tanzania na kuwataka watanzania kumuunga mkono Mhe. Rais Dkt. Magufuli katika harakati za kuijenga Tanzania mpya.

Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa  Dkt.Ali Mohamedi Shein akiongea leo na wakazi wa Dodoma na watanzania kwa ujumla wakati wa shughuli ya maadhimisho ya Siku ya kumbukumbu ya Mashujaa Tanzania na kusisitiza kuhusu umuhimu wa watanzania kuenzi amani iliyoasisiwa na wazee wetu na kuacha kushiriki katika vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani.

Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa John Samweli Malechela akiongea leo na wakazi wa Dodoma na watanzania kwa ujumla wakati wa shughuli ya maadhimisho ya Siku ya kumbukumbu ya Mashujaa Tanzania na kumshukuru kwa kusimamia na kutekeleza ahadi zilizowahi kutolewa na hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikiwemo kuhamishia serikali Mkoani Dodoma.

Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa akiongea leo na wakazi wa Dodoma na watanzania kwa ujumla wakati wa shughuli ya maadhimisho ya Siku ya kumbukumbu ya Mashujaa Tanzania na kumuahidi Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwa atahakikisha anasimamia utekelezaji wa maagizo ya kuitaka Serikali ihamie mjini Dodoma.

Mnara wa Kumbukumbu ya Mashujaa baada ya kuwekwa kwa silaha za asili za mashujaa na maua

Baadhi ya wananchi wakifuatilia shughuli ya maadhimisho ya Siku ya kumbukumbu ya Mashujaa Tanzania katika viwanja vya Mashujaa vilivyopo mjini Dodoma.
(Picha na Hassan Silayo)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwasili katika viwanja vya Mashujaa vilivyopo mjini Dodoma wakati wa shughuli ya maadhimisho ya Siku ya kumbukumbu ya Mashujaa Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiweka silaha za asili kwenye Mnara wa Mashujaa leo Mkoani Dodoma wakati wa shughuli ya maadhimisho ya Siku ya kumbukumbu ya Mashujaa Tanzania
(Picha na Ikulu)
Na: Immaculate Makilika- Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amewaasa watanzania kudumisha amani iliyopo ambayo ilipatikana baada ya Mashujaa mbalimbali kuipigania na hata kujitoa uhai wao kwa ajili ya Taifa.

Akizungumza leo, wakati akihutubia wananchi mara baada ya kumaliza shughuli za maadhimisho ya Siku ya kumbukumbu ya Mashujaa  iliyofanyika katika viwanja vya Mashujaa vilivyopo mjini Dodoma.

Rais Magufuli alisema kuwa maadhimisho ya kumbukumbu za Mashujaa  ni muhimu kwa vile watu hao walijotoa kwa ajili ya kulitetea taifa.

“Wakati tunawakumbuka waliotangulia mbele za haki, sisi tuliobaki tudumishe amani hii, kama ambavyo wao waliotutangulia hawakujali dini zao bali taifa hili” alisema Rais Magufuli.

Aliongeza kuwa nchi ya Tanzania imebaki kuwa kisiwa cha amani, na amani hiyo isichezwe  bali ijengwe na kudumishwa kwa umoja na mshikimamano ili kusaidia kuitangaza nchi zaidi.

Aidha, viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Dkt.Ali Mohamedi Shein, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili  Mheshimiwa Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa John Samweli Malecela nao wapewa fursa ya kuzungumza na wananchi kuhusu maadhimisho hayo ya kumbukumbu ya siku ya Mashujaa.

Viongozi hao, wamesisitiza umuhimu wa kudumisha amani iliyopo na kusema kuwa ni jukumu la wananchi  wote kuhakikisha  hawashiriki katika vitendo vitakavyosababisha   uvunjifu wa amani.

Ambapo, waliwataka wananchi kuwaombea Mashujaa wote waliofariki katika vita mbalimbali wakiwa  katika  harakati za kulifanya Taifa la Tanzania kuwa huru.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, alisema kuwa atahakikisha anasimamia utekelezaji wa agizo la Rais la kuitaka Serikali kuhamia mjini Dodoma.

“Nahamia Dodoma mwezi wa tisa,na nitakapohamia mawaziri wote lazima wanifuate. Katika hili nitasimamia kwa nguvu zote” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Awali, Mheshimiwa Rais Magufuli alisema kuwa atahakikisha katika kipindi cha utawala wake, Serikali inahamia mjini Dodoma, kwa vile Rais wa Awamu ya kwanza Mwl. Julius Nyerere alionesha nia ya kufanya hivyo.

 Aliongeza  kuwa  kwa sasa mji wa Dodoma unaweza kukidhi mahitaji hayo ya Serikali kwa kutumia  miundombinu iliyopo, hata hivyo Serikali inaendelea kujenga miundombinu mipya.

Maadhimisho ya kumbukumbu za Mashujaa hufanyika Julai 25, ya kila mwaka, kwa   kufanya  maombolezo ya Mashujaa waliopigana katika vita mbalimbali katika harakati za kutetea uhuru wa nchi ya Tanzania.

 Maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika kwa mara ya kwanza mjini Dodoma, ambapo Rais John Pombe Magufuli alikuwa mgeni rasmi, ikiwa ni mara yake ya kwanza kuhudhuria maadhimisho hayo kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa