Home » » SERIKALI YAANZA KUINADI DODOMA

SERIKALI YAANZA KUINADI DODOMA

Sehemu ya Mji wa Dodoma

SERIKALI imewaomba wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), wakawekeze katika kuujenga mji huo ili uendane na hadhi ya makao makuu ya nchi.
Jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya WAziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), Paskasi Muragili walikutana na wafanyabiashara hao, ambako waliwaorodheshea fursa mbalimbali, zinazopatikana Dodoma katika kipindi hiki, ambacho Serikali imetangaza kuhamia huko.
Huduma ya maji
Katika mkutano huo, wafanyabiashara hao walielezwa kuwa Dodoma hakuna shida ya maji, kwani kwa sasa zinazalishwa mita za ujazo milioni 65 kila siku na zinatozumika ni mita za ujazo milioni 40 tu; na hivyo kuwepo na ziada ya mita za ujazo milioni 20.
Sekta ya umeme Kwa upande wa umeme, Muragili kuwa kituo cha Tanesco cha Zuzu kinazalisha megawati 48 kwa siku na zinazotumika ni megawati 25 tu, hivyo kuwepo na ziada ya umeme ya megawati 23, “hivyo hofu ya tatizo la maji na umeme halipo, njooni mjenge viwanda.”
Katika mkutano huo, Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) iliazimia kwamba inaunga mkono azimio la Rais John Magufuli la kuhamia Dodoma, na wameahidi kuchangamkia fursa zilizoko katika mkoa huo. Lakini, pia wameiomba Serikali kuweka vivutio mbalimbali kwa wale wote ambao watakuwa tayari kuwekeza mkoani humo.
Mhagama katika maelezo yake kwa wafanyabiashara hao, alisema mchakato wa kutunga sheria za kufanya Dodoma uwe makao makuu ya Serikali, uko kwenye hatua za mwisho na lengo hasa ni kutaka kila jambo litakalofanywa katika mji huo kusimamiwa na sheria moja.
Alisema sheria hiyo itaeleza vivutio vitakavyowekwa kwa wawekezaji, watakaoenda kuwekeza katika mji huo. Pia alisema sheria hiyo itaweka mfumo ambao sekta binafsi, itashirikiana na Serikali katika kuijenga Dodoma.
“Nawaomba mchangamkie fursa hii katika kupanua wigo wa biashara yenu, mimi niko tayari kushirikiana na nyinyi usiku na mchana; semeni mmepanga nini, mnataka nini, sisi tupo tayari ili mradi msibaki nyuma katika kuijenga Dodoma,” alisema Mhagama.
Alisema Watanzania wanatakiwa kumuunga mkono Rais Magufuli kuhamia Dodoma kwa vitendo, na akaeleza kuwa ndani ya Serikali wanaendelea na taratibu za kuhama, hivyo wafanyabiashara wanaweza kwenda sasa hivi kwa ajili ya kuweka miunbombinu mbalimbali.
Waziri huyo alisema Serikali inapoenda kuhamia Dodoma kujenga makao makuu ya nchi, inawahitaji sekta binafsi kwani serikali peke yake haiwezi kujenga mji huo peke yake.
Alisema tayari ameiagiza CDA kuacha urasimu kwa wawekezaji, ambao wataonesha nia ya kuwekeza mkoani humo.
“Nimeagiza kama mfanyabiashara anahitaji kiwanja apewe ndani ya wiki moja, kama unataka kujenga hoteli njoo upate kiwanja, lakini ukiendeleze sio kikae miaka 20 bila kuendelezwa,” alisema na kusisitiza kuwa Serikali inataka kuwepo na spidi kali inayoongozwa na uzale ndo katika kuwekeza Dodoma.
Fursa zilizopo Dodoma
Awali, Muragili alitaja fursa mbalimbali zilizoko katika mji wa Dodoma kuwa ni ujenzi wa nyumba za kupangisha kwa kuwa kutakuwa na idadi kubwa ya watu ambao watahamia makao makuu ya nchi.
Alisema ujenzi wa majengo makubwa kwa ajili ya upatikanaji wa ofisi nao unahitajika haraka kwa kuwa kwa sasa hakuna majengo hayo katika mji huo.
“Hakuna majengo mengi ya ofisi yenye hadhi ambayo yanaendana na makao makuu ya nchi, serikali haiwezi kujenga ni jukumu lenu nyinyi sekta binafsi,” alisema.
Mkurugenzi huyo alitaja fursa nyingine kuwa ni ujenzi wa hoteli, kwani kwa sasa Dodoma kuna hoteli nne tu ambazo zina hadhi ya nyota tatu.
Alisema hakuna hoteli hata moja yenye hadhi ya hoteli tano ; na hivyo akasema ni fursa kwa wafanyabiashara kwenda kujenga hoteli hizo zenye hadhi, ziendanane na makao makuu ya nchi. Alisema mkoa pia hauna maghala ya kuhifadhi vyakula, ambavyo vitaagizwa na wafanyabiashara kutoka nje ya mkoa ili kutosheleza kuwalisha watu ambao wataongezeka katika mji huo.
Alisema ujenzi wa maghala, unahitajika kwa pia. Kwenye kilimo, pia alisema kunahitajika kilimo cha matunda kwa wingi kutokana na mkoa huo kuwa na maji mengi. Alisema ujenzi wa viwanda pia ni fursa kubwa na akatoa mfano ujenzi wa Kiwanda cha Bia ni wa muhimu mkoani humo kutokana na mkoa huo kuwa maarufu kwa kilimo cha nafaka mbalimbali.
Ujenzi wa maeneo ya burudani yenye hadhi, pia yanahitajika pamoja na viwanja vya michezo mbalimbali ili watu wakimaliza kufanya kazi wawe na sehemu za kupumzika. Alisema kwa kuwa wenyeji wa Dodoma ni wafugaji, kuna haja ya kujenga machinjio ya kisasa ambayo yatasaidia hata nchi kusafirisha nyama nje ya nchi.
Akiongezea kutaja fursa hizo, Waziri Mhagama alisema kunahitajika ujenzi wa shule za msingi na sekondari, ambazo alisema haziwezi kujengwa na Serikali peke yake. “Njooni mjenge shule, ni fursa kubwa,” alihimiza.
Pia alisema ujenzi wa majengo mbalimbali utakuwa mkubwa; hivyo akawataka wafanyabiashara kufanya tathmini kama hapa nchini kuna nondo ambazo zinatosheleza kuhimili ujenzi, unaoenda kufanyika katika mji huo. Hiyo nayo ni fursa kubwa.
Alisema kwa kuwa idadi ya watu itaongezeka hadi kufikia watu milioni moja, ni wazi kuwa kutakuwa na mahitaji makubwa ya mafuta, hivyo akataka wafanyabiashara wajipange kuwekeza katika sekta ya mafuta.
TPSF wamsifu Dk Magufuli
Mwenyekiti wa TPSF, Dk Reginald Mengi alisema Rais Magufuli anatakiwa kuungwa mkono kwa uamuzi mgumu alioufanya wa kuhamia Dodoma baada ya miaka 40 tangu kuasisiwa kwa mpango huo na Serikali.
“Huyu ni Rais ambaye anatembea kwenye maneno yake, anafanya yale anayoyasema, kutekeleza mpango huu ni jambo la ujasiri na amefanya maamuzi magumu, sio jambo rahisi kutekeleza jambo ambalo limeshindikana kwa miaka 40,” alisema.
Aliongeza kuwa wafanyabiashara ni jukumu lao kuwa na macho yanayoona fursa katika mkoa huo na wasisubiri kuhamasishwa na Serikali. Alisema hiyo ni fursa ya kupanua biashara yao na wengine ni fursa ya kuanzisha biashara mpya.
Katika maazimio yao, TPSF ilikubali kwenda kuwekeza mkoani humo, ila wakataka kuwepo na kamati itakayoundwa kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuzungumza maeneo ya uwekezaji, ambayo yatafnaywa na sekta binafsi na yale ambayo yatafanywa na serikali yenyewe.
Shule za Al Muntazir kutua Dodoma
Katika hatua nyingine, uongozi wa Shule za Al Muntazir za jijini Dar es Salaam umesema utajenga shule zake mjini Dodoma katika kile walichokiita kuunga mkono uamuzi huo wa Dk Magufuli.
Shule za Al Muntazir zinamilikiwa na Taasisi ya Kiislamu ya Khoja Shia Ithnasheri Jamaat (KSIJ) na zinatoa elimu kwa watoto kuanzia umri wa miaka mitatu hadi 18 kwa kutoa elimu katika ngazi za elimu ya awali, elimu ya msingi, sekondari na sekondari ya juu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Khoja Shia Ithnasheri Jamaat, Azim Dewji, wameitikia mwito wa Rais Magufuli wa serikali yake kuhamia Dodoma na wao kama taasisi inayojihusisha na masuala ya kijamii ikiwamo elimu, wameona ni vyema wakaanzisha shule mkoani Dodoma ili kusaidia jamii ya huko.
“Tumeamua kuunga mkono uamuzi wa Rais John Magufuli wa kuhamishia serikali mkoani Dodoma. Kama unavyojua taasisi yetu inamiliki shule za Al Muntazir kwa hiyo, katika elimu tumekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii nchini. Kwa msingi huo tumeona tunayo fursa ya kusaidia kuwezesha Dodoma kuwa makao makuu ya nchi,” alisema Azim Dewji.
Alieleza kuwa katika kutekeleza azma hiyo, wiki hii uongozi wa Khoja Shia Ithnaasheri Jamaat utakwenda mkoani Dodoma kuonana na Mkuu wa Mkoa huo, Jordan Rugimbana kwa ajili ya kujadiliana naye kuhusu kupewa eneo kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo.
Aliongeza kuwa wanaamini katika muda mfupi watakamilisha ujenzi wa shule hizo ili kutoa fursa kwa wakazi wa Dodoma na watumishi wa umma ambao watakuwa wamehamia katika makao makuu ya nchi, kupeleka watoto wao kupata elimu.
Shule hizo za Al Muntazir, zinafundisha kwa kufuata mitaala ya kitaifa na ya kimataifa kupitia Cambridge International Schools na ni shule pekee yenye cheti cha Taasisi ya Kimataifa ya Viwango (ISO) katika ukanda huu.
Shule hizo zina wanafunzi zaidi ya 4,500 kila moja ikiwa na wanafunzi zaidi ya 1,000. Pia shule hizo zimeajiri zaidi ya wafanyakazi 500 katika nafasi mbalimbali, ikiifanya Al Muntazir kuwa moja ya shule kubwa katika ukanda huo.

CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa