Na Eleuteri
Mangi-MAELEZO, Dodoma
Serikali imewasilisha
Miswada miwili inayohusu Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serikali wa mwaka 2016 na ule wa Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia wa
mwaka 2016 ambayo imesomwa kwa mara ya pili Bungeni ili ijadiliwe na wabunge.
Awali akisoma Muswada
wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa mwaka 2016,
Wizari wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalim amesema
kuwa madhumuni ya Muswada huo ni kuanzisha Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serikali na kuweka kisheria majukumu yake.
Aidha, Waziri Ummy
amesema kuwa Muswada huo umezingatia masuala mbalimbali ikiwemo kuanzishwa kwa Mamlaka
ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na kuainisha majukumu yake na kuanzisha
Bodi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mambo mengine
yaliyozingatiwa katika Muswada huo ni kubainisha utaratibu wa uteuzi wa Mkemia
Mkuu wa Serikali, majukumu yake na mamlaka yake, kuifanya Mamlaka ya Maabara ya
Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa maabara ya rufaa na msemaji wa mwisho wa Serikali
katika shughuli za uchunguzi wa kimaabara wa kikemia, sayansi jinai na vinasaba
na Muswada huo utawwzesha kuwekwa utaratibu wa kusajili, kuratibu na kusimamia
maabara na shughuli zote za maabara za kikemia, sayansi jinai na vinasaba.
Zaidi ya hayo, Waziri
Ummy amesema kuwa kupitia Muswada huo kitawekwa kifungu maalum chini ya Mamlaka
ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kitakachogharimiwa na Serikali kwa ajili
ya uchunguzi wa vielelezo vya makosa ya jinai, majanga na masuala mengine yenye
maslahi ya taifa ili kuwezesha utekelezaji wa jukumu hilo kwa ufanisi hali
itakayosaidia utoaji wa haki katika vyombo vya maamuzi na kuleta utengamano
katika jamii.
Aidha, Muswada wa pili
uliowasilishwa unahusu Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia wa mwaka
2016 ambapo maoni na ushauri yaliyotolewa na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma
ya Maendeleo ya Jamii yaliyosawilishwa na Jasmin Tisekwa (Mb) kwa niaba ya
Mwenyekiti wakamati hiyo Peter Serukamba amesema kuwa Muswada huo utasaidia
kutungwa kwa sheria ambayo italeta tija
kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Zaidi ya hayo,
Jasmini amesema kuwa Muswada huo utasaidia wanataaluma ya Kemia kukabiliana na
maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja kwa kuzingatia taaluma hiyo kwani ina
mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta za elimu, kilimo, viwanda, sheria,
afya, mazingira na jamii kwa ujumla wake.
Akisoma maoni ya
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Waziri
Kivuli wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ester
Mtiko amepongeza jitihada zinazofanywa
na wataalamu wa kemia katika sekta mbalimbali kwa kuwa wana wajibu mkubwa kwa
maslahi ya taifa kwa ajili ya usalama na kuendeleza maarifa ya kisayansi.
0 comments:
Post a Comment