Home » » Duwasa kutekeleza miradi mikubwa ya maji

Duwasa kutekeleza miradi mikubwa ya maji


Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Maji, Gerson Lwenge, wakati akizindua Bodi ya saba ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa Mji wa Dodoma (Duwasa).
Alisema bodi hiyo ina wajibu wa kuhakikisha inaelekeza nguvu zake kuhakikisha ujio wa Serikali mkoani humu haukwami kwa sababu ya ukosefu wa maji.
Alisema Duwasa ina kazi kubwa kuhakikisha uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma haukwamishwi na ukosefu wa maji. Lwenge alisema wakati huu Serikali inapojipanga kuhamia Dodoma ni vyema mamlaka hiyo ikatatua changamoto zote zinazoweza kusababisha kukwama kwa Serikali kuhamia mkoani humu.
Pia aliitaka mamlaka hiyo kudhibiti upotevu wa maji ili watumiaji wa maji hayo wayapate.
"Mnapoongeza kiasi cha uzalishaji wa maji hakikisheni kuwa kinakwenda sambamba na ubadilishaji wa miundombinu ya kusafirishia maji hayo ili kusababisha maji yote yanayozalishwa kuwafikia wateja wenu," alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Duwasa, David Pallangyo, alisema mradi wa kuzalisha majisafi kwenye Bwawa la Farkwa lililopo wilayani Chemba utakapokamilika mamlaka hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia watu milioni moja.
Alisema kwa kiasi cha majisafi kinachozalishwa sasa katika visima vya Mzakwe, Duwasa ina uwezo wa kuhudumia watu watakaohamia mjini hapa katika siku za mwanzo.
Alisema kwa sasa Duwasa ina uwezo wa kuzalisha jumla ya mita za ujazo wa majisafi 61,500 kiasi ambacho kinatosha kuhudumia wakazi wote wa mji wa Dodoma na zaidi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Duwasa, Balozi mstaafu, Job Lusinde, alisema changamoto inayoikabili mamlaka hiyo kwa sasa ni kuongeza uzalishaji katika Bwawa la Farkwa ili iweze kuhudumia idadi kubwa ya watu watakaohamia mjini hapa.

CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa