Home » » Mfuko wa Mafunzo wa Habari utaweka utaratibu wa maslahi ya waandishi wa habari - Serukamba

Mfuko wa Mafunzo wa Habari utaweka utaratibu wa maslahi ya waandishi wa habari - Serukamba

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba amesema kuwa uanzishwaji wa  Mfuko wa Mafunzo wa Habari utaweka utaratibu wa maslahi ya waandishi wa habari utakaowasaidia kuwa na bima za afya, mikataba inayoeleweka pamoja na kuwaendeleza kimasomo.

Hayo yanesemwa leo Mjini Dodoma na Mwenyekiti huyo alipokuwa akihitimisha kikao cha Kamati hiyo kilichokuwa kikijadili juu ya muswada wa habari ambao kwa mara ya kwanza uliwasilishwa Bungeni mnamo mwezi Septemba mwaka huu.

Serukamba amesema kuwa Kamati hiyo imesikiliza maoni ya kila mmoja na imejitahidi kupitia kifungu hadi kifungu cha muswada huo na Serikali imekubali kuyafanyia mabadiliko baadhi ya maeneo ya muswada huo kulingana na maoni yaliyowasilishwa na wadau mbalimbali.

“Muswada huu utakapokuwa sheria tunategemea kuunda Mfuko wa Mafunzo wa Habari ambao utawaendeleza waandishi wa habari kwa kuwawekea utaratibu wa maslahi yao, utakuwa ni kwa ajili ya waandishi wa habari wote watakaothibitishwa na Bodi ya Ithibati”, alisema Serukamba.

Amefafanua kuwa mfuko huo utawezesha mafunzo kwa wanataaluma ya habari, utakuza programu za uendelezaji maudhui ya ndani ya nchi pamoja na kuchangia utafiti wa maendeleo katika nyanja za habari na mawasiliano ya umma, hivyo, utasaidia kurudisha taaluma ya habari kwenye hali nzuri nchini.

Aidha, ameongeza kuwa sheria hiyo itahakikisha inalinda haki za waandishi wa habari, vyombo vya habari pamoja na wananchi wa kawaida  kwa sababu itaweka  utaratibu juu ya utatuaji wa kesi zinazohusiana na  vyombo vya habari kwa muda mfupi hivyo kusaidia watu  kupata haki zao haraka.

Muswada huo pia umetoa kipindi cha mpito cha miaka mitano kwa wanahabari kujiendeleza kielimu katika taaluma ya habari ili wawe na vigezo vitakavyowawezesha kuwa wanahabari kamili waliobobea kwenye taaluma hiyo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa