Home » » MKUTANO WA TANO WA BUNGE KUANZA KESHO MJINI DODOMA

MKUTANO WA TANO WA BUNGE KUANZA KESHO MJINI DODOMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Na Jacquiline Mrisho na Eleuteri Mangi – MAELEZO, Dodoma


Mkutano wa Tano wa Bunge la 11 wa Bunge la Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania unatarajiwa kuanza kesho Novemba 01 hadi Novemba 11 mwaka huu.

Taarifa hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Spika wa Bunge, Job Ndugai alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya shughuli mbalimbali zitakazofanywa na bunge kutokana na ratiba itakayotolewa kulingana na Kanuni ya 64.

“Hali ya Bunge ni shwari na salama, nawasihi wabunge ambao bado hawajawasili Dodoma waje ili tuweze kuifanya kazi ya kuishauri Serikali”, amesema Mhe. Ndugai.

Spika ameyataja baadhi ya majukumu yatakayotekelezwa katika Mkutano wa Tano wa Bunge la 11 kuwa ni pamoja na kujadili, kupokea na kutoa maoni kuhusiana na muongozo wa kuandaa Bajeti ijayo ambapo katika mjadala huo Serikali itapata ushauri kuhusu vyanzo mbalimbali vya mapato na kupata ushauri kutoka kwa wabunge kuhusiana na vipaumbele ambavyo vitatiliwa mkazo katika uandaaji wa Bajeti ya mwaka 2016/2017.

Kazi zingine zitakazofanyika katika mkutano huo ni pamoja na kipindi cha maswali yatakayoelekezwa kwa Serikali na kupatiwa majibu kutoka wizara mbalimbali na taasisi zake, isipokuwa siku ya Alhamisi ambapo maswali ya papo kwa papo yasiyozidi 10 yataelekezwa kwa Mhe. Waziri Mkuu ambayo atayapatia majibu.

Aidha, Spika amesema kuwa katika mkutano huo, Bunge litapokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na majibu ya Serikali kuhusiana na taarifa hiyo pamoja na taarifa za kamati mbili za fedha ambazo ni Kamati ya Fedha za Serikali na Kamati ya Fedha ya Serikali za Mitaa kuhusu kazi walizofanya kulingana na hesabu zilizokaguliwa na CAG kwa mwaka wa fedha 2014/2015 kwa lengo la kujadili matumizi ya Serikali baada ya matumizi hayo kufanyika.

Vile vile katika mkutano huo Bunge linatarajia kupata siku moja ili wabunge wajadili mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Ulaya (EU) ambao ni muhimu kwa maslahi ya nchi ikitarajiwa wabunge wataishauri Serikali endapo Tanzania iridhie kuingia mkataba huo au isiridhie kulingana na ushauri utakaolewa na wabunge ambapo Serikali itakuwa ndiyo muamuzi wa mwisho wa suala hilo.

Ameongeza kuwa Bunge hilo litapokea Miswada miwili itakayowasilishwa ukiwemo Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba 3 wa mwaka 2016.

Kuanza kwa mkutano huo kunafuatia kumalizika kwa vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge vilivyofanyika kwa muda wa wiki mbili mjini Dodoma ambapo kamati hizo zilikutana na kujadili mambo mbalimbali ya kuishauri Serikali katika azma ya kuwaletea wananchi maendeleo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa