Na Mwandishi Wetu-Dodoma
SERIKALI
imewasilisha mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii
Muswada wa Huduma za Habari ikieleza kuwa ni sheria itakayoleta mageuzi
makubwa nchini.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape
Moses Nnauye alipokuwa akiwasilisha muswada wa sheria hiyo leo mjini
Dodoma ambapo amesema sasa sekta ya habari inakwenda kuwa taaluma
kamili.
Waziri
Nnauye amesema Sheria hii italeta mifumo ya kisasa ya usimamizi wa
sekta ya habari na mifumo ambayo inaweza kugusa au kubadili namna
wanahabari walivyozoea kutenda au kufikirika kwa sasa lakini akasema
sekta hiyo iwe tayari kwa mabadiliko.
“Niwaombe
wanatasnia wenzangu tuwe tayari kwa mabadiliko haya ili taaluma yetu
iheshimike na sisi wenyewe tuheshimike zaidi” alisisitiza Mhe. Nnauye.
Aidha Mhe. Nnauye ametoa wito kwa wadau wote kuunga mkono muswada huo utakaojadiliwa katika Bunge lijalo la Novemba mwaka huu.
“Tuko
hapa kuboresha na sio kusuguana tukae tuiandae tasnia bora zaidi kwa
kupitia na kutoa maoni juu ya Muswaada huu wa Sheria ya Huduma za Habari
2016” alifafanua Mhe. Nnauye.
Ameongeza
kuwa kwa sasa hadi wakati wa Bunge lijalo Serikali ipo tayari kupokea
na kuyafanyia kazi maboresho yatakayolenga kufikia maono ya muswada huu
kutoka kwa wadau ili kuipa heshima stahiki sekta ya habari.
Alisema
kuwa muswada huo licha ya huu utatatua changamoto za kutotambulika kwa
sekta ya habari kama taaluma kamili inayopaswa kuheshimiwa, pia utatatua
changamoto ya kukosekana vyombo madhubuti na huru vya usimamizi wa
tasnia.
Alisema kutokana na hayo muswada unapendekeza kuundwa kwa Bodi ya Ithibati itakayoainisha sifa za mwanahabari na kuwasajili.
Aliitaja
taasisi nyingine inayoundwa kuwa ni Baraza Huru la Wanahabari ambalo
litakuwa na wajibu wa kuandaa na kusimamia maadili ya wanahabari na
watawajibishana wenyewe kwa wenyewe.
Wasomi wanena
Mhadhiri
wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Benson
Bana anasema kuwa kuja kwa sheria hiyo ni jambo la busara kwa sababu kwa
sasa weledi wa uandishi wa habari uko chini.
“Sheria
hii iwe na makali zaidi kwa wanahabari ambao watakiuka utaratibu na
maadili. Hakuna nchi ambako wanahabari wanajiendea tu bila uratibu,”
alisema,
Alisema
ni vyema na ni wakati mauafaka kwa sekta ya habari kuwa taaluma kamili
na kushauri kuwa wanaoitumikia fani hiyo kwa sasa wawe tayari kwa
mabadiliko.
Naye
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, Dkt William John Walwa alisema sheria imekuja wakati
muafaka na inapaswa kutatua changamoto za fani hiyo.
0 comments:
Post a Comment