Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma
Serikali
imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3 katika Bajeti ya mwaka wa fedha
2017/2018 kwa ajili ya kukarabati, kupanua na kumalizia ujenzi wa
mabweni mapya pamoja na majengo ya utawala katika baadhi ya magereza
nchini.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba ameyathibitisha hayo
leo mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mhe. Hawa Mwaifunga (Mbunge
wa Viti Maalumu) lililohoji kuhusu mpango wa Serikali katika kuhakikisha
hali za magereza katika Mkoa wa Tabora zinaboreshwa.
Mhe.
Mwigulu amesema kuwa katika kuhakikisha hali ya magereza nchini
inaboreshwa ili kuhakikisha haki za binadamu zinatekelezwa, Serikali
inaendelea na mpango endelevu wa kufanya upanuzi wa magereza ya zamani
na kujenga magereza mapya katika kila Wilaya ambapo utekelezaji huo
unafanyika kulingana na upatikanaji wa fedha.
“Katika
mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga bilioni 3 katika Bajeti kupitia
Fungu la Maendeleo kwa ajili ya kukarabati magereza ambapo shilingi
milioni 185 kati ya bajeti iliyotengwa ni kwa ajili ya kukarabati
magereza ya Mkoa wa Tabora, hivyo tunategemea magereza ya mkoa huo
yatakuwa katika hali nzuri”, amesema Mwigulu.
Ameongeza
kuwa Serikali inatambua msongamano wa mahabusu uliopo katika magereza
mengi nchini na kuongeza kuwa Jukwaa la Haki Jinai limekuwa likifanya
vikao vya kuharakisha kesi ambazo upelelezi wake haujakamilika ili
kupunguza msongamano huo.
Aidha,
Waziri Mwigulu amesema kuwa Serikali inahakikisha Askari Wapelelezi
wanapewa mafunzo kulingana na kazi yao ili waweze kufanya ukamataji wa
watuhumiwa kwa kuzingatia uzito wa ushahidi wa muhusika na kuepusha
malalamiko ya kubambikiwa kesi na kujikuta Serikali inatumia gharama
nyingi kuwatunza mahabusu hao.
Kuhusu
usalama wa askari, Waziri Mwigulu amesema kuwa Serikali itaendelea
kuliwezesha Jeshi la Polisi nchini kwa kuwapa vitendea kazi bora na
kuwajengea uwezo wa mafunzo askari hao ili waweze kukabiliana na matukio
ya uhalifu dhidi ya wanananchi na mali zao pamoja na uvamizi wa vituo
vya polisi nchini.
“Hadi
kufikia Septemba 2016 Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata silaha 19
kati ya 23 zilizoporwa kutoka kwa askari waliovamiwa wakiwa wakitekeleza
majukumu yao hatua inayoonesha jeshi la Polisi linavyofanya kazi kwa
umakini” alisema Mwigulu.
Kwa
upande mwingine, Waziri Mwigulu ametoa rai kwa wananchi kutoa taarifa
katika vituo vya Polisi vilivyo karibu pindi wanapokuwa na shaka juu ya
watu wasiowatambua au kufanya kazi zisizoeleweka ili kuwahakikishia
wananchi usalama wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kimaendeleo.
0 comments:
Post a Comment