Home » » BOT YASITISHA KUWEKA DHAHABU KAMA HAZINA YA RASILIMALI ZA KIGENI.

BOT YASITISHA KUWEKA DHAHABU KAMA HAZINA YA RASILIMALI ZA KIGENI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.

Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imesitisha kuweka dhahabu kama hazina ya rasilimali za kigeni kwa sababu ya kuyumba kwa bei ya madini hayo katika soko la dunia na kusababisha uwezekano wa kupunguza thamani ya hazina ya rasilimali ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Igunga Mhe. Dalaly Kafumu aliyehitaji kufahamu sababu za Serikali kukataa kutunza dhahabu safi katika Benki Kuu wakati Tanzania ni nchi mojawapo inayozalisha dhahabu safi.

Mhe. Kijaji amesema kuwa jukumu la msingi la Benki Kuu ni kuandaa na kutekeleza Sera ya Fedha inayolenga kuwa na utulivu wa bei kwa ajili ya ukuaji endelevu wa uchumi wa Taifa hivyo ili kufanikisha azma hiyo Benki Kuu inadhibiti ongezeko la ujazi wa fedha kwa kutumia nyenzo mbalimbali zikiwemo za kuuza dhamana na hati fungani za Serikali pamoja na kushiriki katika soko la jumla la fedha za kigeni kati ya mabenki.

“Katika kutekeleza jukumu lake la msingi, Benki Kuu hutunza hazina ya rasilimali za kigeni zinazotosha kuagiza bidhaa nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne lakini kwa muda mrefu sasa Benki Kuu ya Tanzania haiweki dhahabu kama sehemu ya rasilimali hizo kutokana na kuyumba kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia”, alisema Mhe. Kijaji.

Naibu Waziri huyo ametoa mfano wa kushuka kwa bei ya dhahabu katika soko la Dunia ambapo dhahabu ilishuka kutoka dola 1,745 za kimarekani katika mwezi Septemba 2012 hadi dola za kimarekani 1,068 kufikia mwezi Desemba 2015.
  
Mhe. Kijaji amefafanua kuwa hazina ya rasilimali za kigeni zinaweza kuwa dhahabu – fedha (monetary gold) au fedha za kigeni ambapo uamuzi kuhusu hazina itunzwe vipi unazingatia vigezo mbalimbali vikiwemo vile vya kudumisha thamani, wepesi wa kubadilisha pamoja na faida inayopatikana kwa kuwekeza hazina hiyo.

Aidha, Mhe. Kijazi amesema kuwa ununuzi na uuzaji wa madini ya dhahabu unahitaji ujuzi maalum ambapo kwa kuzingatia jukumu la msingi la Benki Kuu inaonyesha dhahiri kuwa Benki hiyo haijajijengea uwezo katika eneo la biashara ya madini hayo.

Mwisho.


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa