Home » » MWAKA MMOJA WA RAIS MAGUFULI: HONGERA KUTIMIZA NDOTO YA MWALIMU NYERERE YA KUIHAMISHIA SERIKALI DODOMA.

MWAKA MMOJA WA RAIS MAGUFULI: HONGERA KUTIMIZA NDOTO YA MWALIMU NYERERE YA KUIHAMISHIA SERIKALI DODOMA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Na: Daudi Manongi-MAELEZO.

NDOTO ya miaka zaidi ya 40 ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Serikali ya Tanzania imeanza kutimia ndani ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano. Jambo ambalo linastahili kupongezwa na wenye mapenzi mema na nchi ya Tanzania.
Uamuzi wa kuhamishia Serikali kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Dodoma limekuwepo tangu mwaka 1973 chini ya chama cha Tanganyika African National Union (TANU), huku Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ikiundwa kwa lengo kubwa la kupanga mji, kuishauri na kuisaidia Serikali ili ihamie huko yalipo makao makuu ya nchi.
Suala hilo, hata hivyo, limesuasua kwa miaka mingi huku jitihada zikionekana kuwa ndogo za kuhamia huko.
Lakini mwezi Julai mwaka 2016 Rais John Pombe Magufuli ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alitoa ahadi kuwa atahakikisha Serikali inahamia Dodoma kabla ya 2020.
Wananchi kwa ujumla, wakiwemo wasomi na viongozi, wamelipokea tamko la Rais Magufuli kwa hisia tofauti, ambapo kuna walioliunga mkono kwa bashasha, wapo waliolipinga, na wengine kufurahishwa na tamko hilo lakini kwa kuhoji kama linaweza kutimia au la!
Na kama litatimizwa, bado wanahoji ni njia zipi zitakazofanikisha zoezi hilo kutokana na ukweli kwamba mara nyingi juhudi hizo zimekuwa zikikwamishwa na siasa.
Lakini kwa nia njema aliyokuwa nayo Rais wa awamu ya Tano Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli baada ya kutoa tamko hilo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitamka kwamba yeye atahamia Dodoma mwezi Septemba mwaka huu (2016) huku akiwataka mawaziri wote kumfuata nyuma baada ya yeye kutangulia.
Walio wengi wamependa tamko hilo na kuliunga mkono suala la kuhamisha wizara  zote za serikali kwenda Dodoma sababu kuu ikiwa kutekeleza suala la maendeleo.

Rais Magufuli pia alitoa sababu mbalimbali za kuhamishia Serikali Dodoma ikiwemo kukamilisha ndoto ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na pia sababu za kiusalama kwani makao makuu ya nchi yeyote lazima yawe katikati ya nchi na hivyo ni vyema kwa serikali yake kuhamia Dodoma, pia sababu nyingine ni kuipisha Dar es Salaam kuwa mji wa biashara hivyo ni fursa ya kujiandaa kwa hilo.

Aidha Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa aliwasisitiza Mawaziri,Manaibu Waziri,Makatibu wakuu na Manaibu wao kumfuata Dodoma ili kutimiza agizo la Rais Magufuli.

Tayari Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA) ipo na imekuwa ikipangiwa bajeti kila mwaka japo hakuna sheria inayoitambua Dodoma kama mji mkuu lakini serikali inatarajia kuwasilisha muswada wa Sheria wa kuufanya mkoa wa Dodoma kuwa Makao makuu hivi karibuni.

Pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akihojiwa kwenye kipindi cha Safari ya Dodoma kinachorushwa na TBC anasema maandalizi ya Ofisi za Serikali Dodoma yamekamilika kwa asilimia 75 na makazi kwa watumishi yamekamilika kwa asilimia 70 hivyo wanaweza kuhamia kwa awamu.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amekaribisha wawekezaji  kuwekeza katika  miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa nyumba za watumishi ambao watajenga nyumba za makazi na kuziuza kwa watumishi wa umma na wananchi.
Amebainisha kuwa mwekezaji atakayekuwa tayari awasiliane na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana ambaye ndiye anayeratibu shughuli hiyo huku akikaribisha wawekezaji wa ujenzi wa Hoteli za kitalii na kawaida.
Aidha, Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Bw. Jordan Rugimbana amesema mkoa wake uko tayari kwa asilimia 70 kuipokea Serikali na tayari wamejipanga kwa majengo ya ofisi, makazi na miundombinu mingine.
Umeme, Maji, Usafirishaji, Makazi na Ofisi vyote vipo vizuri, tumeona sasa Dodoma iko tayari na Serikali inaweza kuhamia kwa asilimia 70 hadi sasa, huduma za afya ambapo kuna hospitali yenye huduma nzuri na  elimu pia.

Kwa kweli ni mipango madhubuti ya Rais John Pombe Magufuli ya ndani ya mwaka mmoja inayofanya utekelezaji huu uwe wenye mafanikio makubwa nchini.
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa alishatekeleza agizo la Rais Magufuli kwa kuhamia Dodoma tarehe 30 Septemba 2016 na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa Serikali na wananchi wa mkoa huo.  Awamu ya kwanza ya kuhamia Dodoma ilitarajiwa  kuanzia Septemba 2016 mwaka huu hadi Februari, ambapo watakaohamia baada ya Mheshimiwa waziri mkuu kuhamia ni mawaziri wote,makatibu wakuu wote, na manaibu katibu wote watahamia, hii ni kwa mujibu wa Mhe. Kassim Majaliwa
“Aidha kila wizara inatakiwa kuwahamisha watumishi wa idara moja au mbili na wakati huo huo wakiendelea kuweka utaratibu mwingine wa idara nyingine kuhamia Dodoma.”
“Awamu ya pili itakuwa Machi 2017 na Agosti 2017. Kipindi hiki kitawapa fursa watendaji wa wizara mbalimbali kuweka bajeti zao katika  mwaka wa Fedha wa 2017 18 na kuendelea kuwahamisha watumishi wake kuja Dodoma. Awamu ya tatu itakuwa kati ya Septemba 2017 na Februari 2018, ambapo wizara zitaendelea na uhamishaji wa wa watumishi wa idara zilizo ndani ya wizara zao,” aliongeza Mhe. Majaliwa.
“Awamu ya nne ni Machi 2018 mpaka Agosti 2018 na awamu ya tano ni Septemba 2018 na Februari 2020. Awamu ya sita ni Machi 2020 na June 2020, itakuwa ni Ofisi ya Rais ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watakuwa wanafika Dodoma.
“Nazishauri Wizara zote katika zoezi hili la kuhamia Dodoma kutumia mifumo ya utunzaji kumbukumbu ya kielektroniki  badala ya kuhama na mafaili yote kutoka Dar mpaka Dodoma kwa kuwa tunataka Dodoma iwe ya kielektroniki”, anasisitiza Waziri Mkuu.
 
Hili ni jambo la kumpongeza Rais Magufuli kwa hatua hii kubwa ambayo imekuwa katika mipangilio kwa muda sasa imeanza utekelezaji wake ndani ya mwaka mmoja wa serikali ya Awamu ya Tano. Heko Rais Magufuli kwa kuamua na kutekeleza, hakika wahenga walisema haja ya mja hunena, muungwana ni vitendo, Kauli hii imethibitika kwa Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tano Mzee wa Hapa Kazi Tu.

 

 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa