Home » » NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI AAGIZA KUKAMILISHWA MARAMOJA KWA MADARASA

NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI AAGIZA KUKAMILISHWA MARAMOJA KWA MADARASA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


Na. Nasra Mwangamilo, Silvia Hyela
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mitaa Mhe. Selemani Jafo ameuagiza Uongozi wa Halmashauri ya  Manispaa ya Dodoma kuhakikisha inakamilisha ujenzi na ukarabati wa  vyumba vya madarasa ya shule ya msingi Chang’ombe, ifikapo tarehe 10 Januari, 2017 kabla ya msimu wa masomo kuanza.
Mhe. Jafo alisema serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imetoa jumla ya shilingi Milioni 192 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 8 vya madarasa na ukarabati wa majengo machakavu katika shule ya msingi Chang’ombe na kuwataka watendaji hao kutumia vizuri fedha hizo zilizotolewa na serikali.
Mhe. Jafo alitoa agizo hilo leo tarehe 03 Novemba, 2016 wakati alipofanya ziara ndogo ya kutembelea Kata ya Chang’ombe ambapo katika ziara hiyo alibaini  changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo zikiwemo upungufu wa madarasa na matundu ya vyoo.
“Natoa agizo kwa Afisa Mipango na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa, ifikapo tarehe 10 Januari, 2017, ujenzi wa majengo haya uwe umeshakamilika na muhakikishe shule yote inakuwa mpya. ”  Alisisitiza Mhe. Jafo.na kuongeza kuwa angependa kazi hiyo ifanyike ndani ya muda na kutojengwa chini ya kiwango cha ubora.
Aidha,  Naibu Waziri  Jafo alionyesha kutoridhishwa na taarifa za ujenzi wa zahanati ya kata ya Chang’ombe ambayo taarifa zilizotolewa zilionyesha kuwa hazikuwa sahihi ukilinganisha na idadi ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo.
“Sijaridhishwa kabisa na ujenzi unaoendelea katika zahanati hii na siamini kama kulikua na usimamizi mzuri, nataka niletewe taarifa inayoambatana na taarifa ya mkandarasi aliyehusika na ujenzi pamoja na mchakato wa manunuzi ya vifaa na maendeleo ya ujenzi ili nijiridhishe na suala hili ”aliagiza Naibu Waziri  Jafo.
Katika ziara hiyo, Mhe. Jafo alipata nafasi ya kuzungumza na watumishi wa Manispaa ya Dodoma na kuwataka  kufanya kazi kwa kuzingatia umuhimu wa mahitaji ya wananchi na kuyawekea kipaumbele mambo ya msingi ikiwamo huduma za afya na elimu lengo likiwa ni kuhakikisha watumishi wa Serikali za Mitaa wanakua watumishi wa mfano kwa utendaji mzuri.
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa