Home » » Uhakiki fedha za Tasaf nyumba kwa nyumba

Uhakiki fedha za Tasaf nyumba kwa nyumba

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


MPANGO wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf), mkoani Dodoma utafanya uhakiki nyumba kwa nyumba kubaini wanufaika hewa wa fedha zake, wanaoendelea kulipwa mamilioni ya fedha wakati hawastahili.
Mratibu wa Tasaf mkoani hapa, Bogit Samhenda, alisema hayo juzi wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa wilaya na halmashauri, kuhusu utekelezaji wa mpango huo wa Tasaf, pamoja na shughuli za serikali.
Samhenda alisema sasa utafanyika uhakiki nyumba kwa nyumba katika wilaya zote saba za Dodoma zinazotekeleza mpango huo, kwani inaonekana baadhi ya wanufaika ni hewa.
“Kuna watu wamehama, wamefariki lakini bado wanaendelea kulipwa, lazima uhakiki ufanyike ili watu hao waondolewe, uhakiki utakuwa endelevu,” alisema.
Alisema katika Awamu ya Tatu ya Tasaf jumla ya kaya 68,730 zilifikiwa na mpango huo na Sh bilioni 33 zilitolewa.
“Wilaya zote saba za mkoa wa Dodoma zinatekeleza mpango huo, Chamwino ilikuwa ya kwanza kuanza kutekeleza mpango huo Januari 2014 na wilaya nyingine zote zilizobaki zilianza Septemba 2014,” alisema na kuongeza kuwa, sasa Chamwino iko katika awamu ya 17, wakati wilaya nyingine sita zimehaulisha awamu 13.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, amepiga marufuku masuala ya siasa kuingizwa kwenye mpango huo wa kunusuru kaya masikini na kutaka kuondolewa wote wasiostahili ili walengwa wanufaike.
Pia, amewataka viongozi wa wilaya ya halmashauri za mkoa wa Dodoma kukaa na kuzungumza lugha moja juu ya utekelezaji wa mpango huo ambapo sasa uhakiki utafanyika nyumba kwa nyumba ili kuwabaini wasiostahili na kuondolewa.
Katibu Tawala wa Mkoa, Rehema Madenge, alisema suala la uhakiki wa walengwa ni lazima lipewe kipaumbele. Alitaka kila mkuu wa wilaya asimamie shughuli hiyo.
 Chanzo Gazeti la Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa