Home » » WIZARA YA AFYA YAANZISHA MAFUNZO YA TIBA SHUFAA.

WIZARA YA AFYA YAANZISHA MAFUNZO YA TIBA SHUFAA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt Hamis Kigwangalla  akijibu hoja mbalimbali kutoka kwa wabunge katika kikao cha saba cha mkutano wa tano wa Bunge la 11 linaloendelea Mjini Dodoma Novemba 9, 2016.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanzisha mafunzo ya Tiba Shufaa (Palliative Care Services) kwa watumishi wa Sekta ya Afya ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa wakati kwa wagonjwa wanaohitaji.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Hamis Kigwangalla ameyathibitisha haya leo mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mhe. Susan Lyimo aliyehitaji kufahamu juu ya mikakati ya Serikali katika kuhakikisha huduma ya Tiba Shufaa inaboreshwa hapa nchini.

Dkt. Kigwangalla amesema kuwa katika kuhakikisha huduma za tiba shufaa zinapatikana hapa nchini, hospitali takribani 35 zikiwemo za Rufaa za kanda za Bugando, KCMC na Mbeya , Hospitali za mikoa pamoja na Hospitali za dini zinatoa huduma hizo.

Ameongeza kuwa huduma hizo pia zimekuwa zikitolewa majumbani kwa wagonjwa wanaokaa karibu na maeneo yenye hospitali zinazotoa huduma hizo ambapo watoa huduma za majumbani husaidia kumfikia mgonjwa moja kwa moja katika maeneo wanayoishi.

“Sera ya kitaifa ya Tiba Shufaa iliyotolewa Mwezi Juni mwaka huu imeagiza mafunzo yafanyike ili kuwajengea uwezo watumishi waliopo katika vituo vya afya na hospitali nchini ili waweze kutoa huduma hiyo” alisisitiza Mhe. Dkt Kigwangalla.

Aidha Wizara hiyo imeanza kutoa mafunzo hayo kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Chama cha Tiba Shufaa pamoja na wadau wengine kwa lengo la kuhakikisha kunakuwa na watumishi watano katika kila kituo cha afya ambao wana uwezo wa kutoa tiba hiyo wakijumuisha madaktari, wauguzi, wafamasia pamoja na maafisa ustawi wa jamii.
 
Tiba Shufaa ni huduma inayotolewa kwa wagonjwa walio katika hatua za mwisho za maisha yao hasa walio na magonjwa yasiyo na uwezekano wa kupona kwa ajili ya kuwapunguzia maumivu makali wanayoyapata kutokana na magonjwa hayo.

MWISHO.
 
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa