Home » » WATAALAMU WA MIPANGO NA MAENDELEO VIJIJINI WAHIMIZWA UADILIFU NA KUJIEPUSHA NA UFISADI

WATAALAMU WA MIPANGO NA MAENDELEO VIJIJINI WAHIMIZWA UADILIFU NA KUJIEPUSHA NA UFISADI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dokta Philip Mpango, amewataka wataalamu wa Mipango na Maendeleo Vijijini kufanyakazi zao kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya rushwa na ufisadi ili kuwawezesha wananchi hususan waishio vijijini kunufaika na huduma yao ili kujikwamua kiuchumi na kuodokana na umasikini
Dokta Mpango ametoa rai hiyo wakati wa mahafali ya 30 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kilichoko eneo la MIYUJI mkoani Dodoma, ambapo wahitimu 1,641 wakiwemo wanaume 796 na wanawake 845 wametunukiwa tuzo zao katika kozi 11 zinazohusu Mipango, Maendeleo, Fedha na uwekezaji.
Amesema kuwa ubunifu na upangaji mzuri wa mipango ya maendeleo vijijini utaharakisha nia ya serikali ya kuwaondolea wananchi wake umasikini hivyo kuboresha maisha yao
Waziri huyo wa Fedha na Mipango, amewahimiza wahitimu hao kuja na mawazo mapya au njia mbadala za kukabiliana na changamoto za  kukuza shughuli za biashara vijijini, hasa ukosefu wa mikopo na mitaji, bima, mfumo dume pamoja na mfumo duni wa uzalishaji na ukosefu wa masoko.
“Ninawaasa wahitimu wetu muwe wazalendo na mfanyekazi kwa bidii kokote mtakako kwenda ili muwe kioo cha chuo hiki kwasababu Tanzania yetu inawataka muwe wabunifu na kukataa kujihusisha na mambo yanayohatarisha amani, usalama na umoja wetu kama watanzania” aliongeza Dkt. Mpango
Aidha, amevishauri vyombo vya habari nchini kuandika habari za changamoto na fursa zinazowakabili wananchi vijijini badala ya kuandika na kutangaza mambo yanayodhalilisha nchi yao kwa kukosekana uzalendo
 “Tumeshuhudia mafanikio makubwa waliyoyapata wakulima kutoka Wilayani Mbulu mkoani Manyara, na Njombe mkoani Iringa ambao wameongeza uzalishaji wa mazao yao ya vitunguu saumu, mahindi na maharagwe pamoja na kuongeza thamani ya mazao hayo, hizo ni habari nzuri za kuandika” alisisitiza
Kwa Upande wake, Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini, Dkt. Frank Hawassi, amesema kuwa wahitimu wa chuo hicho wameandaliwa katika mfumo unaolenga weledi na umahiri utakao wawezesha kutekeleza majukumu yao kwa tija zaidi katika maeneo yao ya kazi.
Amesema kuwa wahitimu hao wameiva na wako tayari kuisaidia nchi kupiga hatua kubwa kimaendeleo katika kutekeleza sera ya uchumi wa viwanda.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho, Prof. Razack Lokina, ameiomba serikali kukisaidia chuo hicho kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa jengo la utawala, hosteli na upungufu wa wahadhiri ili kukiwezesha chuo hicho kuendelea kutoa elimu bora kwa wahitimu wake.
Akizungumza katika mahafali hayo, Mwanafunzi bora wa shahada ya uzamili, Bi. Gemma Mafwolo, amesema kuwa wahitimu wa chuo hicho wameiva na wako tayari kutumika mahali popote hapa nchini kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo ya wananchi vijijini.
 “Tunapenda kukuahidi kuwa tutatumia elimu tuliyoipata kwa manufaa mapana ya taifa letu kwa kuibua, kupanga, kutekeleza, kusimamia, kufuatilia na kufanya tathimini ya mipango na maendeleo katika nyanja zote za maendeleo” alisisitiza Mafwolo
Vilevile ameishukuru serikali kwa kuahidi kutatua baadhi ya changamoto zinazokikabili chuo hicho ikiwemo ukosefu wa sehemu za malazi ya wanafunzi, maeneo ya michezo pamoja na upungufu wa wahadhiri.
Zaidi ya wataalamu wa mipango ya maendeleo vijijini 14,583, wamehitimu mafunzo yao tangu chuo hicho cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kianzishwe mwaka 1980 kikisimamiwa na Wizara ya Fedha na Mkipango.
Katika tukio jingine, waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, amezindua jengo la pili la taaluma la Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini lililojengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 10.3 lenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,250 wanaofundishwa kwa wakati mmoja.
Jingo hilo la ghorofa 7 lina kumbi 4 za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua watu 320 kila mmoja, madarasa 6 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 150 kila moja, chumba kimoja cha maabara ya kompyuta chenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 150 kwa wakati mmoja, ukumbi 1 wa mikuta (80), Stoo 2, kantini 1 na vyumba vya ofisi 32.
Mwisho

 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa