Home » » Wizara ya Afya kuhamia Dodoma siku 14 zijazo

Wizara ya Afya kuhamia Dodoma siku 14 zijazo

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto , Ummy Mwalimu .

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto itahamia Dodoma ndani ya siku 14 zijazo.
Waziri Ummy Mwalimu amesema tayari wizara yake imejiandaa kuhamia Dodoma, kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la serikali kuhamia Dodoma kabla ya 2020.
“Tutahamia Dodoma ndani ya muda wa wiki mbili,” alisema Ummy wakati akifungua semina ya kitaifa ya afya mjini hapa juzi. Aliwatangazia wadau wa afya nchini kwamba atatangaza kabla ya kuhamia Dodoma ni huduma gani zitaendelea kutolewa Dar es Salaam na zile zitakazohamishiwa Dodoma.
Alithibitisha kwamba ofisi yake kama waziri, ya naibu waziri, na Katibu Mkuu wake wa wizara, hazitabaki Dar es Salaam, bali zitakuwa Dodoma.
Kuhamia kwa wizara hiyo Dodoma, itakuwa ni wizara ya tano, uhamisho huyo ulitanguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyehamia Septemba mwaka jana na baadaye akafuata Waziri wa Nchi katika ofisi yake, Jenista Mhagama anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu.
Mawaziri wengine waliohamia Dodoma ni wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene na msaidizi wake, Selemani Jafo pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki.
Kutokana na ratiba iliyotangazwa na Waziri Mkuu mwaka jana, waziri mkuu na mawaziri wote pamoja na makatibu wakuu wa wizara, wanatakiwa kuwa tayari wamehamia Dodoma kufikia Februari 28, mwaka huu.
Ratiba hiyo inaonesha kati ya Machi na Agosti mwaka huu, watendaji wa wizara wanatakiwa kupanga na kutenga bajeti kwa maofisa wao kuhamia makao makuu ya nchi.
 Chanzo Gazeti la Habari leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa