Home » » TAARIFA KWA UMMA SERIKALI YAFAFANUA MIKOPO KWA VIJANA, MALIPO ADA KWA FEDHA ZA KIGENI

TAARIFA KWA UMMA SERIKALI YAFAFANUA MIKOPO KWA VIJANA, MALIPO ADA KWA FEDHA ZA KIGENI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. TAARIFA KWA UMMA

SERIKALI YAFAFANUA MIKOPO KWA VIJANA, MALIPO ADA KWA FEDHA ZA KIGENI

Dodoma, Jumatano, 1 Februari, 2017:  

Serikali imetoa ufafanzi kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa mikopo kwa vijana na malipo ya ada kwa fedha za kigeni. Ufafanuzi huo umetolewa mjini hapa leo wakati wa kikao cha pili katika Mkutano wa Sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  

                                 Kuwainua Vijana Kiuchumi

Akijibu hoja kuhusu namna vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini wanavyoweza kufaidika kiuchumi, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Anthony Mavunde, amesema Serikali imetenga fedha za kutosha kupitia mifuko mbalimbali kuwawezesha vijana kwa mitaji na mafunzo ya ujasiriamali ili kuwainua kiuchumi.

Ameongeza kuwa vijana wenyewe ndio wanaopaswa kuchangamkia fursa hizo na pale wanapojiunga katika vikundi mbalimbali wamekuwa wakipewa mikopo kwa ajili ya mitaji. Alitoa mfano wa jinsi Serikali ilivyowawezesha vijana waliojiunga na kuwekeza katika viwanda vidogo vya maziwa na chaki mkoani Simiyu.

Amewataka pia Wabunge na Halmashauri zote nchini kuendelea kupigania kutengwa maeneo maalum katika sekta mbalimbali kwa ajili ya kuwapatia vijana na kutengwa kwa asilimia 5 ya mapato ya Halmashauri kwa maendeleo ya vijana

        Ada kwa Fedha za Kigeni

Serikali imesema, ingawa haijapokea malalamiko yoyote kuhusu wananchi wasioridhihwa na mtindo wa kutakiwa kulipa malipo ya ada kwa fedha za kigeni katika baadhi ya shule na vyuo, lakini imesisitiza kuwa wale wanaotoza ada kwa fedha za kigeni wanakiuka Sheria.

Akitoa ufafanuzi huo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhandisi Stella Manyanya amesema kwa mujibu wa kifungu cha 28 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT), 2006, fedha inayopaswa kutumika kwa malipo ya huduma nchini ni Shilingi ya Tanzania. Ameviagiza vyuo na shule nchini kuacha kutoza ada kwa fedha za kigeni na kuhimiza wananchi watakaobainika kufanya hivyo kutoa taarifa Serikalini.

Si Tatizo Kutumia Majengo UDOM

Serikali imesisitiza kuwa baadhi ya Wizara zilizoanza kutekeleza agizo la kuhamia Dodoma kutumia baadhi ya majengo kwa muda kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) hakutaathiri shughuli za chuo.
                                         
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama.  Waziri Jenista amesisitiza kuwa baadhi ya Wizara zitatumia majengo ya UDOM kwa sababu mengi ya majengo hayo yalikuwa hayatumiki kwa sasa kwa shughuli za chuo hicho na hakutakuwa na muingiliano na shughuli za chuo.

                                 Mradi wa Mabilioni Maji Dar

Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Dar es Salaam imeanza kutekeleza mradi wa usambazaji wa maji utakaogharimu Dola za Marekani milioni 32.772 ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Exim ya China. Mradi huo utahusisha sehemu yote ya jimbo la Kawe, Dar es Salaam. Mradi huo utachukua miezi 15.


Imetolewa na:
Idara-Habari Maelezo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa