Home » » TAARIFA YA SERIKALI TOKA BUNGENI LEO 10/02/2017

TAARIFA YA SERIKALI TOKA BUNGENI LEO 10/02/2017

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Dodoma, Ijumaa, 10 Februari, 2017:  

Serikali imefafanua masuala mbalimbali yaliyoulizwa na Wabunge ikiwemo masuala ya utozaji wa kodi wa hoteli (Hotel levy), suala la wanunuzi wa korosho kutolipwa kwa wakati, ahadi ya kuboresha maisha ya wavuvi na wakulima, utekelezaji wa REA III.Ufafanuzi huo umetolewa leo Bungeni Mjini hapa.

Kukusanya Kodi katika Hoteli za Kitalii

Serikali imesema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Hoteli, Halmashauri haziruhusiwi kukusanya kodi katika hoteli za kitalii. Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo ametoa kauli hiyo leo Bungeni akisema kuwa Halmashauri zinaruhusiwa kwa mujibu wa kifungu cha 26(3) cha Sheria hiyo kukusanya ushuru wa hoteli katika nyumba za kulala wageni zilizokoko ndani ya halmashauri.

Ameongeza kuwa, halmashauri zinaruhusiwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 kifungu cha 6(u) kukusanya ushuru wa huduma (Service levy) katika hoteli za kitalii zinazoendesha shughuli zake ndani ya halmashauri kwa kiwango kisichozidi asilimia 0.3 ya mapato ghafi ya Taasisi husika.

Wanunuzi wa Korosho kutolipa Wakulima Kwa wakati

Serikali imesema kuwa, kupitia Bodi ya Korosho imekuwa ikihimiza wanunuzi kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Mamlaka husika. Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Tate Ole-Nasha.

Amesema kwamba, Serikali kupitia Sheria ya Korosho Na.18 ya Mwaka 2009 Kifungu Na.17 na Kanuni za mwaka 2010 Kanuni ya 33 itaifungia kampuni yoyote kufanya biashara ya korosho nchini endapo itakiuka Sheria na Kanuni ikiwemo ya kutowalipa wakulima kwa wakati ili kubaki na makampuni yanayotii Sheria.

Ahadi ya Kuboresha Maisha ya Wavuvi na Wakulima

Kuhusu suala la kuboresha maisha ya wavuvi na wakulima, Naibu Waziri Ole-Nasha amefafanua kuwa, Serikali imeendelea na jitihada zake za kuwajengea mazingira mazuri wakulima na wavuvi nchini kwa kuhakikisha kuwa, gharama kubwa za pembejeo na vyombo vya uvuvi zinapungua ili waweze kuzipata kwa bei nafuu kwa kutenga kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya ruzuku ya zana za uvuvi, na jumla ya shilingi bilioni 26.99 kwa ajili ya ununuzi wa mazao katika bajeti ya Wizara ya mwaka 2016/17.

Aidha, amesema kuwa, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula umetengewa shilingi bilioni 15.0 na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko shilingi bilioni 8.95. Pia amefafanua kuwa, Serikali haikopeshi wavuvi, bali inaweka mazingira wezeshi kwa wavuvi hao kupata mikopo yenye riba nafuu ambapo, kupitia Benki ya Rasilimali (TIB) imeweka Dirisha la Kilimo Kwanza kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima na wavuvi. Ameongeza kuwa, Serikali imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ambayo baadhi ya majukumu yake ni kuwapatia wakulima na wavuvi mikopo yenye riba nafuu.

Utekelezaji wa Mradi wa REA III

Serikali imesema kwamba, jumla ya Vijiji 37 ambavyo havijapatiwa umeme katika jimbo la muheza na vitongoji 137 vinatarajiwa kupatiwa umeme kupitia Mradi wa Umeme wa Vijijini (REA) Awamu ya Tatu. Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani ameeleza kuwa, utekelezaji wa Mpango wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kwa nchi nzima unatarajiwa kufanyika kwa mgawanyo wa vipengele vitatu vya Densification, Grid Extension pamoja na Off-Grid Renewable.

Imetolewa na:

Idara ya Habari-MAELEZO.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa