Home » » Wafanyabiashara wa Pombe za Kienyeji Wanatakiwa Kuwa na Leseni

Wafanyabiashara wa Pombe za Kienyeji Wanatakiwa Kuwa na Leseni

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma

Wafanyabiashara wa Pombe za Kienyeji wanatakiwa kuwa na leseni ya kufanya biashara hiyo ambayo hutolewa na Halmashauri.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo ameyasema hayo, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Najma Giga juu ya Serikali imejipangaje kukabiliana na tatizo la ulevi wa kupita kiasi kwa pombe za kienyeji pamoja na sheria ya vileo ya mwaka 1969 kuwa ya zamani hivyo kutokidhi mabadiliko ya hali halisi ya vileo.

“Pombe za kienyeji zimeanishwa katika kifungu cha 2 cha tafsiri katika Sheria ya Vileo, Sura ya 77 ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, wafanyabiashara wote wanatakiwa kuwa na leseni ambayo inatolewa na Halmashauri,” alifafanua Jafo.

Aliendelea kwa kusema kuwa, biashara hiyo hairuhusiwi kufanyika katika muda wa kazi. Muda unaoruhusiwa kisheria ni kuanzia saa 12:00 jioni hadi saa 5:00 usiku kwa siku za Jumattu hadi Ijumaa na kuanzia saa 05:00 asubuhi hadi saa 06:00 usiku kwa siku za Jumamosi, Jumapili na Sikukuu.

Vile vile  amesema kuwa unywaji wa pombe kupita kiasi ni tabia ya mtu ambayo inawezekana kabisa haitokani na mapungufu ya Sheria.
Hata hivyo Wakuu wa Mikoa na Wilaya wameagizwa kusimamia taratibu za uendeshaji wa biashara za vileo na kuchukua hatua kwa watumiaji na wafanyabiashara wanaobainika kukiuka Sheria hiyo.

Aidha amesema kuwa, endapo ipo haja ya kuifanyia marekebisho Sheria ya vileo, Serikali itakuwa tayari kupokea mapendekezo kwa eneo ambalo litaonekana kuwa na mapungufu ili kufanyiwa marekebisho kupitia Bunge.

Jafo ametoa wito kwa Watanzania wote kutumia muda wao kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo kwa ustawi wa Taifa zima. Aidha Serikali haitasita kuchukua hatua kwa wanywaji pombe wasiozingatia utaratibu pamoja na wazururaji wakati wa kazi.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa