Home » » CHUO CHA MIPANGO- DODOMA CHAHIMIZA MATUMIZI YA TAFITI KUKABILIANA NA ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIA NCHI

CHUO CHA MIPANGO- DODOMA CHAHIMIZA MATUMIZI YA TAFITI KUKABILIANA NA ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIA NCHI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 Na Benny Mwaipaja,WFM


Wadau wanaofanya tafiti mbalimbali za Maendeleo ya uchumi nchini hasa maeneo ya vijijini kuhusu Mabadiliko ya Tabia nchi wametakiwa kuwasilisha matokeo ya tafiti hizo Serikalini na katika Mashirika mengine ya Maendeleo ili matokeo yake yafanyiwe kazi na kusudio la tafiti hizo liweze kufikiwa.

Rai hiyo imetolewa Jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini - Dodoma, Prof. Razack Lokina wakati wa Mkutano uliohusu mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kiuchumi uliozihusisha Taasisi za  Serikali na  Binafsi pamoja na Washirika wa Maendeleo.

Amesema Chuo cha Mipango kimekuwa kikifanya kazi zake vijijini, zikiwemo za tafiti mbalimbali na matokeo hayo huwasilishwa katika ngazi husika ikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia mazingira pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kutumia matokeo hayo kwa manufaa ya maendeleo ya jamii hasa vijijini.   

“Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia nchi ambao umejadili mbinu mbalimbali za kukabiliana na athari za kiuchumi zinazotokana na Mabadiliko hayo, umetokana na andiko la Wanafunzi wa Chuo hicho waliokwenda katika mafunzo kwa vitendo vijijini na kushuhudia namna mabadiliko ya tabia nchi yalivyoathiri maendeleo ya wananchi”. Alifafanua Prof. Lokina

Tayari Chuo kina mradi ujulikanao kama Chololo Ecovillage unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) Mkoani Dodoma, ambao huwafundisha wanakijiji njia bora za uzalishaji mali, hivyo kuwafanya baadhi ya Wananchi waliokuwa wanakosa chakula, kutokana na hali ya Ukame wa Mkoa huo kuanza kupata mazao ya kutosha na kuongeza pato lao.

Naye Mkuu wa Chuo hicho cha Mipango ya Maendeleo vijijini- Dodoma,  Dkt. Frank Hawassi, amezitaka Taasisi na Mashirika ya umma na Binafsi kuunganisha nguvu katika kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia nchi kwa kuwa kama juhudi hazitachukuliwa athari zake zitampata kila mmoja.

Aidha, amesema hakuna nchi inayoweza kufanikiwa kukabiliana na tatizo hilo bila kushirikiana hata kama nchi hiyo imeendelea kwa kiasi kikubwa. Pia Jamii inapaswa kujua kuwa hata matatizo ya wafugaji, wakulima na wengine kuhusu ardhi ni matokeo ya athari za Mabadiliko ya Tabia nchi, hivyo kila mmoja  anatakiwa kuwa chachu ya utunzaji wa mazingira, ili maendeleo yanayopatikana yawe endelevu.

Ameongeza kuwa Chuo cha Mipango Dodoma kinatoa nafasi kwa wadau kote nchini kukitumia kikamilifu katika kutatua changamoto za kimazingira kwa kuwa ipo Idara iliyo na jukumu la kushughulikia suala la Mazingira na Mabadiliko ya Tabia nchi. 

Kwa upande wake aliyekuwa Balozi wa Umoja wa ulaya nchini Tanzania  Tim Clarke, ambaye ameongoza timu ya washirika wa Maendeleo katika Mkutano huo ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini kujitahidi kuwahamasisha wananchi kutumia Nishati mbadala ikiwemo Gesi ili kupunguza kasi ya uharibifu wa misitu kwa kukata miti kwa ajili ya kupata Mkaa.

Vilevile ametoa rai kwa Serikali kuwa karibu na jamii na kuwaelimisha kuhusu kutunza mazingira katika shughuli zao za kila siku za kujipatia kipato ili kusaidia kulinda mazingira ya asili yatakayochochea kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa