Home » » SAMIA ATOA MAAGIZO MAZITO KWA VIONGOZI DODOMA

SAMIA ATOA MAAGIZO MAZITO KWA VIONGOZI DODOMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi na wadau wa mkoa wa Dodoma kwenye mkutano wa kazi, ambapo Taarifa ya Awali ya mkoa wa Dodoma na utekelezaji wa uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma, iliwasilishwa katika ukumbi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dodoma, uhakikishe unaondoa vitendo vya ukiritimba kwa baadhi ya watendaji wa serikali, ambavyo vinaweza kusababisha ucheleweshaji au kukwamisha ujenzi wa miji mipya mikubwa mitano ya kisasa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Samia alitoa kauli hiyo jana wakati akifanya mazungumzo na viongozi wa Mkoa wa Dodoma baada ya kupokea taarifa ya Kikosi Kazi, kilichoundwa na serikali kwa ajili ya kuratibu shughuli mbalimbali za serikali kuhamia Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na ofisi yake, Makamu wa Rais amesema ni muda muafaka sasa hivi kwa uongozi wa mkoa kujiimarisha na kujipanga ipasavyo katika kupokea wawekezaji wenye nia njema ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali mkoani humo hasa wakati huu ambao serikali inahamia humo.
Ameonya kuwa wawekezaji matapeli kamwe wasipewe nafasi ya kuwekeza Dodoma na ametaka uongozi wa mkoa kuwa makini makundi hayo ili wasije kuvuruga mipango ya serikali ya kujenga Makao Makuu ya kisasa katika Manispaa ya Dodoma.
Pia ameuagiza uongozi wa mkoa, kulinda na kuendeleza maeneo yote yenye uoto wa asili ili yasije yakaharibiwa kutokana na uwekezaji utakaofanyika mkoani humo.
Alisema amefurahishwa na kasi ya uongozi wa Mkoa wa Dodoma, jinsi unavyojipanga katika kuhakikisha azma ya serikali ya kuhamia Dodoma inafanikiwa kwa haraka ikiwemo utengaji wa maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na huduma za kijamii.
Kuhusu maeneo ya wafanyabiashara ndogo, Makamu wa Rais amewataka viongozi wa Mkoa wa Dodoma wahakikishe wanatenga haraka maeneo maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ili nao wanufaike na mpango wa serikali kuhamia mkoani humo.
“Ni muhimu maeneo yote yatakayotengwa kwa ajili wafanyabiashara ndogo yawe huduma zote za msingi ili kusaidia wafanyabiashara hao waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi,” alisisitiza Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais alisisitiza kuwa ni muhimu kwa uongozi wa Mkoa wa Dodoma, kuwashirikisha viongozi wa wafanyabiashara ndogo kuhusu maeneo yatakayotengwa ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara hao kupewa maeneo yasiyofaa wa ajili ya shughuli zao.
Awali, kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais kuzungumza na viongozi wa mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alimweleza Makamu wa Rais mipango na mikakati ya mkoa huo kuhusu azma ya serikali ya kuhamia Dodoma ikiwemo kuimarisha huduma za msingi ikiwemo afya, miundombinu, maji na elimu.
Alisema mpaka sasa kazi ya kuainisha maeneo mbalimbali kwa ajili ya uwekezaji, makazi na mahali ambapo ofisi za serikali na za mabalozi zitajengwa umeshakamilika.
Alisema wataendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali, mashirika ya kimataifa na mabalozi ili kuhakikisha maeneo yaliyotengwa yanaendelezwa haraka.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa