Home » » PRESS RELEASE YA YALIYOJIRI KATIKA KIKAO CHA TANO CHA MKUTANO WA SABA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA LEO MJINI DODOMA.

PRESS RELEASE YA YALIYOJIRI KATIKA KIKAO CHA TANO CHA MKUTANO WA SABA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA LEO MJINI DODOMA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

SERIKALI YAFAFANUA KUSHAMIRI KWA BIASHARA YA VYUMA CHAKAVU, MPANGO WA KUUNDA BODI MPYA YA TUMBAKU NA UTENGAJI ASILIMIA MAALUM KWA WANAFUNZI KUTOKA TANZANIA BARA NA ZANZIBAR

Dodoma,Jumanne, 11 April, 2017.

Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu kushamiri kwa Biashara ya vyuma chakavu,Mpango wa kuunda bodi mpya ya Tumbaku na Utengaji wa asilimia maalum kwa wanafunzi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, Ufafanuzi huo umetolewa leo Bungeni mjini Dodoma.

Kushamiri kwa Biashara ya Vyuma Chakavu

Serikali imesema kuwa, imekwishaandaa Rasimu ya Muswada wa Sheria itakayoweka  bayana taratibu na mfumo wa usimamizi na udhibiti wa biashara ya chuma chakavu katika hatua mbalimbali za uzalishaji,ukusanyaji,usambazaji,uuzaji na uyeyushaji wake kwa kuzingatia uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa manufaa ya Taifa.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuongezeka kwa mahitaji ya vyuma chakavu hapa nchini na duniani kwa ujumla na kubainisha maeneo yaliyoathirika sana kuwa ni mifumo ya kusafirisha Umeme,Reli na Barabara.


Akifafanua kuhusu hoja hiyo, Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles Mwijage  amesema Muswada huo umeweka bayana adhabu itakayotolewa kwa mtu atakayebainika kuharibu miundombinu.

Aidha Mhe.Mwijage ametoa wito kwa Wananchi wote kutoa taarifa pindi waonapo mtu anayehujumu miundombinu kwa namna yoyote ile.




Mpango wa kuunda Bodi mpya ya Tumbaku.

Serikali imesema kuwa, iko katika maandalizi ya kuunda Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Tumbaku haraka iwezekanavyo na Wananchi watajulishwa kupitia tamko la Serikali mara baada ya taratibu kukamilika.

Naibu Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi Mhe.William Ole Nasha amesema kuwa, Serukali ilivunja Bodi ya Tumbaku kwa lengo la kufanya maboresho katika utendaji kazi wake.

Ameongeza kuwa, hatua ya kuvunja Bodi hiyo haihusiani na kusitisha shughuli zinazotekelezwa katika Kilimo cha Tumbaku kwani wapo wataalamu wanaondeleza utekelezaji wa mpango uliopo wa kuendeleza zao la Tumbaku nchini.

Aidha kwa kuzingatia kuwa wakulima wanahitaji huduma muda wote hasa kipindi hiki cha kuelekea masoko ya tumbaku kwa msimu wa 2017/18,Serikali kupitia mrajis wa vyama vya Ushirika nchini imeshateua timu nyingine ambayo ipo Mkoani Tabora ikiendelea kuratibu na kusimamia masuala mbalimbali ya wakulima ikiwa ni pamoja na kuandaa upatikanaji wa pembejeo kwa msimu ujao.

Serikali kuendelea kutenga fedha kwa wahitaji wa Mikopo ya Elimu ya juu.

Serikali imesema kuwa itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya juu kwa kuzingatia Sheria,kanuni na taratibu na miongozo itolewayo mara kwa mara na serikali kupitia bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya juu.

Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi,Teknolojia na Ufundi Mhe. Stella Manyanya amesema kuwa utoaji wa Mikopo unazingatia muombaji awe raia wa Tanzania,muhitaji,mlemavu au yatima na mabaye amedahiliwa katika elimu ya juu na mwenye kuchukua programu za vipaumbele vya Taifa kama Sayansi, Hisabati,uhandisi  wa Gesi na Mafuta, Sayansi za Afya na Sayansi za Kilimo na Maji.

Aidha Mhe.Manyanya amesema kuwa katika Mwaka wa 2015/16 Serikali ilitoa kiasi cha Tsh.bilioni 480 kugharamia Mikopo pamoja na ruzuku kwa wanafunzi wapatao 124,358.

Ameongeza kuwa  Serikali inalifanyia kazi suala la wanafunzi kutopata Mikopo  ili kuongeza idadi ya wanafunzi.


 Imetolewa na:

Idara ya Habari-MAELEZO.

 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa