Home » » WAZIRI UMMY: UGONJWA WA EBOLA HAUJAFIKA TANZANIA

WAZIRI UMMY: UGONJWA WA EBOLA HAUJAFIKA TANZANIA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Na. Eliphace Marwa
MAELEZO
29.5.2017
 
SERIKALI imesema kuwa Tanzania bado haijafikiwa na ugonjwa hatari wa Ebola na kuwatoa hofu wananchi baada ya mlipuko wa ugonjwa huo kuikumba nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amewataka wananchi kutokuwa na hofu bali wachukue tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo, kwani hadi sasa hakuna mtu aliyethibitishwa kuugua ugonjwa huo hapa nchini.
Waziri Ummy amewataka wananchi hususani wanaoishi mikoa ya karibu na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiwemo mikoa ya Mwanza, Kagera, Kigoma, Rukwa, Katavi na Songwe wanapaswa kuwa makini kwani tayari mlipuko wa ugonjwa wa Ebola umethibitishwa DRC.
“Mpaka sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imethibitika kuwa na wagonjwa 43 na wagonjwa wanne wamekwisha poteza maisha hadi sasa,” alisema Waziri Ummy.
Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa Wizara itahakikisha inashirikiana na wadau mbalimbali wa afya ili kupata mbinu za kudhibiti ugonjwa huo usiingie nchini.
“Kupitia wataalam wa afya waliopo katika mipaka ya nchi serikali itakuwa ikitoa taarifa za mara kwa mara ya namna uzuiaji wa ugonjwa huo kwa wananchi na wanapata elimu ya kutosha ya kujikinga na virusi vya Ebola”, alisema Waziri Ummy.
Waziri Ummy aliongeza kuwa wananchi wanashauriwa kutoa taarifa pamoja na kupata elimu kuhusu ugonjwa wa Ebola kwa kupiga simu namba 117 na kupata huduma bila ya malipo kwa mitandao yote.
Aliongeza kuwa Serikali imeendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu wake walioko mipakani ikiwa ni pamoja na utoaji wa vifaa vya kujikinga na ugonjwa huo pamoja na vidonge kwa wataalamu hao walioko mipakani.
“Serikali tayari imeagiza mashine nne kwa ajili ya kufanya vipimo katika mipaka yetu pamoja na viwanja vya ndege na bandari zetu na tutahakikisha kila mgeni anayewasili nchini kutokea Congo anasajiliwa,” alisema Waziri Ummy.
Ugonjwa wa Ebola unasababishwa na kugusa majimaji yanayotoka kwa mgonjwa mwenye virusi vya Ebola na mizoga na dalili za ugonjwa huu zinatokea baada ya siku mbili pindi mgonjwa anapopata maambukizi ya ugonjwa huo zikiwemo kutokwa na damu sehemu za puani, masikioni na homa kali.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa