Home » » FEDHA ZA DAWA MOTO

FEDHA ZA DAWA MOTO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene

SERIKALI imetoa siku saba kwa halmashauri ambazo hazijamaliza matumizi ya fedha hasa kwa upande wa ununuzi wa dawa na vifaa tiba kutoa maelezo kwa njia ya maandishi ni kwanini fedha hizo hazijatumika kama zilivyopangwa wakati wananchi wakilalamika kukosa dawa na kwanini wasichukuliwe hatua.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza kwenye mkutano wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya uliomalizika mjini hapa. Agizo hili linawahusu Makatibu Tawala wa Wilaya na Mikoa yote hapa nchini.
Alisema hali ya matumizi ya fedha katika halmashauri nyingi ni changamoto kubwa kwani licha ya wananchi kukosa dawa na vifaa tiba bado kuna halmashauri zina fedha nyingi kwenye akaunti zao na kuvuka mwaka wa fedha na wakiwa na bakaa. Waziri huyo alisema si lengo la serikali kuwepo na fedha zinazovuka mwaka, hasa ikizingatiwa kuwa katika mwaka wa fedha 2016/17 fedha za mfuko wa pamoja wa Afya (HBF) zilifika kwenye mikoa na halmashauri kwa wakati lakini bado wananchi hawana dawa na vifaa tiba.
Aliwaagiza makatibu tawala wa mikoa yote 26 kwamba halmashauri zote ambazo hazijamaliza matumizi ya fedha hasa upande wa ununuzi wa dawa na vifaa tiba zitoe maelezo. “Nawapa wiki moja kuanzia leo zilete maelezo kwa maandishi ni kwanini fedha hizo hazijatumika kama zilivyopangwa ilihali wananchi wanalalamika kukosa dawa na ni kwa sababu zipi wasichukuliwe hatua,” alisema Waziri Simbachawene.
Alisema mwaka 2015/16 fedha hizo zilitolewa bila kujali matokeo kwa nia ya kuzitaka halmashauri kutumia fedha hizo kuboresha huduma kabla hazijaanza kupimwa kwa matokeo, isipokuwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia zilitolewa kwa njia ya matokeo kwa kutumia utaratibu huo. “Si halmashauri zote zilifanikiwa kupata fedha hizo, makatibu tawala wa mikoa wanatakiwa kuhakikisha halmashauri zinafikia vigezo vilivyowekwa ili kusitokee tena halmashauri kupoteza fedha hizo,” alisema.
Hata hivyo, alisema serikali kwa kushirikiana na wadau, wameamua kuanzia mwaka huu wa fedha 2017/18, serikali itaanza kupeleka moja kwa moja kwenye akaunti za vituo vya kutolea huduma za afya ikiwa ni katika hatua ya kuimarisha huduma za afya ngazi za msingi na kudhibiti upotevu na uchelewaji wa fedha kuwafikia watoa huduma.
Alisema katika kufanya kwa vitendo falsafa ya Tamisemi mpya imekuja na utaratibu wa kuwa na mkataba wa ufanisi wa kazi kwa viongozi. “Sitasikia halmashauri imevuka mwaka huu tulioumaliza na mabilioni ya fedha kuingia mwaka 2017/18, sitasikia malalamiko yanayohusu lugha chafu na isiyo na staha kwa wateja na dawa muhimu zinapatikana kwa wakati wote. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wadau wa maendeleo, kutoka Ubalozi wa Uswis, Thomas Teuscher alisema sekta ya afya nchini inakabiliwa na changamoto nyingi na serikali ijitahidi kufanya maboresho ili kuboresha huduma za afya kwa ujumla hasa katika suala la uwajibikaji.
CHANZO HABARI LEO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa