Home » » KUBENEA KORTINI KWA KUMDUNDA MBUNGE

KUBENEA KORTINI KWA KUMDUNDA MBUNGE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma.

MBUNGE wa Jimbo la Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Saed Kubenea amefi kishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini kujibu shtaka la kumshambulia mbunge mwenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Juliana Shonza.
Kubenea alifikishwa mahakamani hapo jana mchana, na anatetewa na mawakili watano. Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, James Karayemaha, Wakili wa Serikali Beatrice Nsana alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Julai 3, mwaka huu kwenye Viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma.
Wakili huyo alidai Kubenea alifanya kosa hilo ikiwa ni kinyume na kifungu cha sheria namba 240 cha sheria ya makosa ya jinai sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho Mwaka 2002.
Kubenea alikana shtaka hilo, na Hakimu Karayemaha alisema dhamana ya mshtakiwa iko wazi na masharti ya dhamana ni kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini dhamana ya Sh milioni moja na mdhamini atatakiwa kuwa na barua ya Mtendaji wa Kijiji au Kata.
Alikamilisha masharti ya dhamana na kudhaminiwa. Juzi, wabunge saba wa Chadema walikamatwa na Polisi mkoani hapa na kuhojiwa kwa siku mbili kuhusu shambulio dhidi ya Shonza ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu.
Hao ni Suzan Kiwanga (Mlimba), Kubenea (Ubungo), Cecilia Pareso (Viti Maalumu), Frank Mwakajoka (Tunduma), Joseph Selasini (Rombo) na Pauline Gekul (Babati Mjini).
 CHANZO HABARI LEO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa