Home » » SPIKA NDUGAI APONGEZWA BAADA YA KUSHINDA NAFASI YA MWENYEKITI WA MASPIKA KATIKA MABUNGE YA JUMUIYA YA MADOLA BARANI AFRIKA

SPIKA NDUGAI APONGEZWA BAADA YA KUSHINDA NAFASI YA MWENYEKITI WA MASPIKA KATIKA MABUNGE YA JUMUIYA YA MADOLA BARANI AFRIKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai akipongezwa na Naibu Spika wa Cameroon, Mhe. Monjowa Lifaka baada ya kushinda nafasi ya Mwenyekiti wa Maspika na Viongozi wa Bunge katika Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Barani Afrika. Uchaguzi huo umefanyika leo katika Mkutano wa Maspika wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Barani Afrika uliomalizika leo Mjini Abuja.
Ofisi ya Bunge inapenda kuuarifu umma kuwa Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai (Mb), leo amechaguliwa kuwa Mwenyekiti  wa Maspika na Viongozi wa Bunge katika Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Barani Afrika. Uchaguzi huo umefanyika  katika Mkutano wa Maspika wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Barani Afrika uliomalizika leo Mjini Abuja.

Kwa wadhifa huo, Mhe Ndugai ataongoza Maspika wenzake toka Mabunge na Mabaraza ya kutunga Sheria  63 yaliyoko katika nchi 18 za Jumuiya ya Madola kwenye Bara la Afrika. Wadhifa huo ni wa miaka miwili kuanzia sasa hadi mwaka 2019 kutakapofanyika uchaguzi mwingine.

Nchi wanachama wa Umoja wa Mabunge Barani Afrika ni pamoja na Afrika  ya Kusini, Botwana, Cameroon ,Ghana, Kenya, Lesotho,   Msumbiji, Mauritius, Malawi, Nigeria, Namibia, Rwanda, Seychelles, Sierra Leone, Swaziland, Tanzania, Uganda na Zambia.

Akizungumzia uchaguzi huo,  Mhe Ndugai amesema "Kwa hakika nawashukuru Maspika wenzangu kwa kunipa dhamana hii ya kuwa Mwenyekiti wao, ni heshima kwangu binafsi lakini zaidi Kwa Tanzania. Ni matumaini yangu kwamba Bunge letu litaendelea kung'ara kitaifa na kimataifa tukiwa Bunge moja lenye Upendo na mshikamano".

Huu ni wadhifa wa nne kwa Mhe. Ndugai katika masuala ya Bunge kwenye medani ya Kimataifa. Amewahi kuwa Mwakilishi wa Nchi za Afrika Mashariki katika Kamati ya Utendaji ya Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Duniani mwaka 2008-2011, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii ya Umoja wa Mabunge ya Afrika, Pacific na Carribbean na Jumuiya ya Ulaya  mwaka 2011-2014 na Rais wa Baraza la Mabunge ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC – PF)
Imetolewa na: 
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano 
Ofisi ya Bunge 
DODOMA 
 27 Julai 2017.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa