Home » » WAKURUGENZI ANDAENI MAZINGIRA BORA KWA AJIRA MPYA – WAZIRI SIMBACHAWENE.

WAKURUGENZI ANDAENI MAZINGIRA BORA KWA AJIRA MPYA – WAZIRI SIMBACHAWENE.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tamisemi Mhe. George Simbachawene (kwanza Kulia) akisalimiana na Wakina Mama wa Kijiji cha Msangambuye wakati wa Ziara yake Wilayani Mpwapwa katika Jimbo la Kibakwe.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tamisemi Mhe. George Simbachawene(mbele) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Msangambue, Kata ya Mtera Tarafa ya Rudi wakati wa Ziara yake Katika Jimbo la Kibakwe.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tamisemi Mhe. George Simbachawene(mbele) akitoa maelekezo kwa Wazee wa Kijiji cha Msangambuye wakati wa Ziara ya Kikazi Jimboni Kibwakwe.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tamisemi Mhe. George Simbachawene(mbele) akizungumza na mwanafunzi wa darasa la kwanza Yusta Mwanshinga katika shule ya Msingi Msangambuya alipopita kuwasalimia wanafunzi wa shule hiyo wakati wa ziara yake.

 Mama Theresia Costantine Komba (kushoto) akimshkuru Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tamisemi Mhe. George Simbachawene kuwatembelea katika Kijiji cha Chinoje. 
 
Na. Nteghenjwa Hosseah, Kibakwe.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tamisemi Mhe. George Simbachawene amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote Nchini kuandaa mazingira rafiki kwa watumishi wapya wanaopangiwa katika Halmashauri zao.

Simbachawene ameyasema hayo ikiwa ni wiki moja tangu kutangaza ajira mpya za Walimu wa Masomo ya Hisabati na Sayansi wapatao 3,081 wa ngazi ya Shahada na Stashahada ambao wamepangiwa kwenye Halmashauri mbalimbali Nchini.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Msangambuya wakati wa Ziara yake ya Kikazi Wilayani Mpwapwa katika Jimbo la Kibakwe Mhe. Simbachawene amesema watumishi wengi wapya wanakatishwa tamaa na mazingira mabovu wanayoyakuta katika Halmashauri zao na hali hiyo huwatia hofu ya kuendelea kukaa katika maeneo hao.

Unakuta mtumishi anafika Halmashauri malipo yake hayajaandaliwa zaidi ya mwezi mzima, kisha anapangiwa kwenye Kata mbayo hata hajawahi kuifahamu hapo awali na hapewi hata maelekezo ya ziada ya namna ya kufika katika Kituo chake na unakuta wenyeji wake katika Kata na Shule hawana taarifa za ujio wa mtumishi huyo hivyo mtumishi anahangaika mpaka anakosa ari ya kufanya kazi katika kituo chake kipya alisema Simbachawene.

“Ninahitaji Kila Halmashauri kuandaa Malipo stahiki kwa ajili ya walimu wanaoendelea kuripoti hivi sasa katika maeneo mbalimbali, Usafiri wa kuwapeleka katika vituo vyao vya Kazi, mapokezi stahiki kwa uongozi wa Kata pamoja Shule sambamba na kuhakikisha anapata makazi bora ya kuishi katika eneo lake jipya la Kazi”.

Sitaelewa Halmashauri ambayo itashindwa kuzingatia maagizo haya kwa namna yeyeote ile na ntaendelea kufuatilia mazingira ya mapokezi ya watumishi hawa, sitaki mtumishi yeyote ashindwe kufanya kazi yake kwa ufanisi kwa sababu ya mazingira magumu anayokutana nayo wakati wa kuripoti kazini, Aliongeza.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Mpwapwa Bi. Eliachi Macha alisema Halmashauri imeandaa mazingira mazuri kwa ajili ya mapokezi ya walimu wapya na pia watahakikisha wanatekeleza Maagizo yote ili watumishi wote waweza kufanya kazi za ujenzi wa Taifa na kuleta matokeo chanya.

Naye Diwani wa Kata ya Mtera Mhe. Amon Kodi ambaye alishiriki katika ziara hii alimpongeza Waziri Simbachawene kwa kazi kubwa anayoendelea kufanya katika Kata yao, Jimbo la Kibakwe na Taifa kwa Ujumla na kumshkuru kwa kufanikisha utekelezaji wa Miradi ya ujenzi wa bweni la Mtera Sekondari, ukarabati wa zahanati ya kisima pamoja na ukarabati wa matundu ya vyoo vya Shule vya Msingi Msangambuya.

Mhe. Simbachawene yupo katika ziara ya Kikazi Wilayani Mpwapwa, Jimbo la Kibakwe na ametembelea Kijiji cha Msangambuya, Chamsisili pamoja na Chinoje.
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa