Home » » AKUTWA AMECHIJWA KAMA KUKU NYUMBA YA SANGOMA

AKUTWA AMECHIJWA KAMA KUKU NYUMBA YA SANGOMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


MSICHANA mkazi wa Kigoma, Mariam Said (17) ameuawa na shingo yake kutenganishwa na kiwiliwili, Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, alisema jana.
Mwili wa msichana huyo, alisema zaidi Kamanda Mambosasa, ulikutwa kwenye nyumba ya mganga wa kienyeji katika kitongoji cha Chang’ombe kilichopo kijiji cha Chamwino Ikulu, wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

Kamanda Mambosasa alisema mkasa huo ulitokea juzi saa 4 usiku katika kijiji hicho, ambapo Polisi ilikuta mbali na shingo ya marehemu kutenganishwa na kiwiliwili, sehemu zake za siri zilichomwa moto.

Mambosasa alisema mwili wa marehemu huyo ulikutwa katika nyumba ya mganga wa kienyeji aitwaye Ashura Matha na ambaye amekuwa akijihusisha na shughuli hizo bila kuwa na kibali.

Alisema kuwa polisi ilibaini kuwa mganga huyo amekuwa akijihusisha na vitendo vya upigaji ramli chonganishi pamoja na kulaza wagonjwa katika nyumba hiyo bila kuwa na kibali cha kutoa tiba za asili.

Kufuatia tukio hilo, Kamanda Mambosasa alisema polisi wanawashikiliwa watu 11 kwa tuhuma za mauaji hayo, ikiwamo Ashura na wasaidizi wake.

Pia alisema wanawashikilia wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika nyumba ya mganga huyo, ulipokutwa mwili wa marehemu.

Kamanda huyo alisema kuwa Jeshi la Polisi mkoani Dodoma linaendelea na uchunguzi zaidi na watuhumiwa watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.


“Hivi sasa tupo katika uchunguzi wa kubaini huu mwili wa huyo marehemu ambaye inasemakana alikuwa ni mkazi wa Kigoma ulifikaje nyumbani kwa mganga huyu,” alisema.

Aliwataka wakazi wa kijiji hicho kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo linapofanya uchunguzi wa tukio hilo, na kuwafichua wote waliohusika na mauaji hayo.

Katika tukio jingine, Mkazi wa kijiji cha Ntyuka Manispaa ya Dodoma, Masumbuko Nyerere (24) amefariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi cha mchanga.

Mambosasa alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi, pia saa moja asubuhi katika kijiji hicho, ambapo mrehemu aliangukiwa na kifusi cha mchanga na kupoteza maisha.

Alitoa rai kwa Wizara ya madini pamoja na mazingira kutembelea maeneo hayo na kutoa elimu kwa wananchi ambao wamekuwa wakijihusisha na uchimbaji wa mchanga, ili kuondoa majanga kama hayo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa