Home » » BALOZI WA TANZANIA NCHINI UTURUKI AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO

BALOZI WA TANZANIA NCHINI UTURUKI AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Mhe. Prof. Elizabeth Kiondo, Balozi Mteule wa Tanzania nchini Uturuki akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Mheshimiwa Recep Tayyip Erdoǧan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki. 
Mhe. Balozi Kiondo akiagana na Mheshimiwa Rais Erdoǧan, baada ya kufanya mazungumzo kuhusu mahusiano ya Tanzania na Uturuki. 
Picha ya pamoja.


Mhe. Prof. Elizabeth K. KIONDO, Balozi wa Kwanza Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uturuki Jumatano ya tarehe 16 Agosti 2017, amewasilisha Hati zake za Utambulisho pamoja na zile za Kukoma kwa Muda wa Mtangulizi wake kwa Mheshimiwa Recep Tayyip Erdoǧan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki. Kitendo hicho kinamfanya Mhe. Kiondo kuwa Balozi wa kwanza mkaazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini humo.

Katika hafla hiyo Mhe. Balozi Kiondo alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Rais Erdoǧan kuhusu namna ya kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili katika maeneo ya uwekezaji, biashara, afya, Elimu, na mengineyo. Aidha, Mhe. Balozi Kiondo alimfahamisha Mheshimiwa Rais Erdoǧan kuwa Ubalozi utakuwa kiungo muhimu katika kuongeza kasi ya utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa wakati wa ziara yake nchini Tanzania mwezi Januari 2017 ambapo mikataba na makubaliano yapatayo tisa yalisainiwa.

Kufunguliwa kwa Ubalozi mpya wa Tanzania nchini Uturuki na kuanza kufanya kazi kunatoa fursa muhimu kwa wananchi wa mataifa hayo mawili kuongeza shughuli za kiuchumi hususan biashara kwa manufaa ya pande zote mbili.

Mhe. Balozi anatoa rai kwa Watanzania kujipanga vizuri na kuchangamkia fursa mbalimbali hususan za kibiashara zinazotokana na kuendelea kuimarika kwa mahusiano kati ya Tanzania na uturuki.
Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 17 Agosti 2017.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa