Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Wakuu wa Mikoa inayolima zao la pamba nchini kwenye makazi yake mjini Dodoma Septemba 9, 2017. Kulia kwake ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba, watatu kulia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo na wanne kulia ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Maimuna Tarishi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa 10 inayolima pamba
nchini wasimamie zao hilo kwa karibu ili kuinua uzalishaji wake na
kuwaongezea kipato wananchi.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni (Ijumaa, Septemba 8, 2017) wakati
akizungumza na wakuu hao wa mikoa kwenye kikao alichokitiisha mjini
Dodoma kujadili mbinu za kufufua zao hilo. Wakuu
wa mikoa walioitwa kwenye kikao hicho ni kutoka mikoa ya Shinyanga,
Singida, Kagera, Tabora, Morogoro, Mara, Mwanza, Simiyu, Katavi na
Geita.
“Serikali
imeamua kufufua mazao makuu matano ya biashara ambayo ni pamba, chai,
kahawa, korosho na tumbaku na leo nimetaka nianze na ninyi wakuu wa
mikoa ili mwende mkawasimamie watu wenu tunapokaribia kuanza msimu
mpya,” alisema.
Waziri
Mkuu alisema Serikali imeamua kusimamia kilimo cha pamba kuanzia
maandalizi ya shamba, kupanda, matumizi ya pembejeo na dawa, kuvuna na
kutafuta masoko na akawataka wasimamie katika maeneo yao ili kilimo cha
zao hilo kiweze kubadilika.
“Kuna
maafisa kilimo kwa kila Halmashauri iliyoko kwenye mikoa yenu. Maafisa
kilimo hawa lazima wahusike kikamilifu. Moja ya majukumu yake kwa cheo
chake, kazi kubwa aliyonayo ni kusimamia zao la pamba. Kama hajafanya
kazi hiyo, usiridhike kuwa na afisa kilimo wa aina hiyo,” alisema.
“Ni
lazima kila mmoja awe na mpango kazi, ausimamie na atoe matokeo ya kuwa
zao hili limefanikiwa katika eneo lake. Tunataka zao hili lichukue
nafasi yake ya namba moja. Heshima ya “Dhahabu Nyeupe” lazima irudi
lakini pia ni vema mkumbuke kuwa zao la pamba ni uchumi, zao la pamba ni
siasa katika mikoa yenu,” alisisitiza.
Kikao
hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles
Tizeba; Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI; Bw. Suleiman
Jafo, Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo, Mrajis
wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Tito Haule na Mkurugenzi Msaidizi wa
Uhamasishaji Mazao, Bw. Beatus Malema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 DODOMA,
JUMAMOSI, SEPTEMBA 9, 2017.
0 comments:
Post a Comment