Home » » MASHAMBA 21,000 KUFANYIWA UTAFITI

MASHAMBA 21,000 KUFANYIWA UTAFITI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MASHAMBA 21,071 ya wakulima yanatarajiwa kufanyiwa utafiti ili kukusanya takwimu rasmi za uzalishaji katika sekta ya kilimo nchini.

Kati ya mashamba hayo, 19,158 ni Tanzania Bara na 1,913 ya Zanzibar.
Akifunga mafunzo ya wadadisi na kuzindua ukusanyaji wa Takwimu za Kilimo kwa mwaka 2016/17 mkoani Dodoma, Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Maria Mashingo, alisema ukusanyaji takwimu hizo ulitarajiwa kuanza jana katika mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani.

Dk. Mashingo alifafanua zaidi malengo ya utafiti huo ni kutoa makadirio ya uzalishaji wa mazao makuu ya kilimo na maeneo yaliyolimwa pamoja na kupata taarifa za mifugo katika mikoa.

Katika kuhakikisha takwimu sahihi zinapatikana, Dk. Mashingo aliwataka wadadisi, wasimamizi na wote walioshiriki katika mafunzo hayo kufanya kazi hiyo kwa weledi na kwa ushirikiano mkubwa.

Hata hivyo, alisema serikali haitasita kumchukulia hatua mtendaji yeyote ambaye atakwamisha au kuleta uzembe katika ukusanyaji takwimu hizo muhimu kwa Taifa.

Dk. Mashingo pia aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kushirikiana na maofisa kilimo na mifugo wa mikoa walioshiriki mafunzo hao, kuhakikisha ukusanyaji takwimu hizo unafanikiwa kwa kiwango cha juu katika mikoa na halmashauri zao.
Alitoa wito kwa wakuu wa kaya watakaochaguliwa kushiriki kwenye utafiti huo, kutoa ushirikiano wa kutosha na hususani kutoa taarifa sahihi kuhusu hali ya uzalishaji wa mazao katika maeneo yao.

Aliwataka watoe taarifa jinsi ambavyo maofisa ugani wanatoa huduma na kuainisha changamoto wanazokumbana nazo, aina ya mbegu wanazotumia na viashiria vyote vilivyoainishwa katika madodoso.

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa, Dk Albina Chuwa, alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wa namna ya kuhoji na kujaza dodoso za wamiliki wa mashamba, kutambua mahali mashamba yalipo kwa kutumia kifaa maalum (GPS).

“Lengo la utafiti wa kilimo katika mwaka 2016/17, ni kutoa makadirio ya kiasi cha uzalishaji wa mazao makuu, idadi ya mifugo, mazao yatokanayo na mifugo na maeneo ya kilimo katika mikoa yote kwa kutumia njia mpya ya utafiti,” alisema. 

Dk. Chuwa alisema makadirio ya idadi ya mifugo na kiasi cha uzalishaji wa mazao, yatasaidia kutoa taarifa za msingi kwa wakulima, wafanyabiashara, wadau wa kilimo na serikali na zitasaidia katika kufanya uamuzi wa mipango ya muda mfupi na mrefu.

Aidha, Dk. Chuwa alisema taarifa zitakazokusanywa katika utafiti huo, zitasaidia katika kuboresha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, hivyo katika kuongeza Pato la Taifa.

Chanzo:Nipashe

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa