Home » » WALIOTIMULIWA CUF WAGONGA MWAMBA KUREJEA BUNGENI

WALIOTIMULIWA CUF WAGONGA MWAMBA KUREJEA BUNGENI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Imeandikwa na Halima Mlacha
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad
BUNGE limeweka wazi kuwa hawatambui wanachama wanane waliovuliwa uanachama na Chama cha Wananchi (CUF) na baadaye kutangazwa kuvuliwa nafasi zao za ubunge na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Taarifa hiyo ya Bunge, imetokana na barua ya CUF kwenda kwa Katibu wa Bunge, Stephen Kigaigai inayomtaka amjulishe Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai, kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu ya kutengua uamuzi wa awali wa chama hicho wa kuwafuta uanachama wa wabunge hao na kuomba Bunge liwatambue kama bado ni wabunge halali.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu taarifa hiyo ya Mahakama Kuu kutengua uamuzi wa awali wa CUF wa kuwafukuza uanachama wabunge hao, Kigaigai alikiri kupokea barua ya chama hicho, lakini alisisitiza kuwa bado chombo hicho hakiwatambui kama wabunge halali.
“Ndio nimeipata barua yao na naanza kuifanyia kazi, ila kifupi tu Bunge haliwatambui watu hao. Sisi tunawatambua wabunge wapya tuliopatiwa orodha na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),” alisisitiza.
Alisema kwa kawaida Bunge hupokea majina ya wabunge wote, wanaoingia ndani ya chombo hicho kutoka NEC na si kwa chama husika, hivyo mpaka sasa hawajapata barua yeyote kutoka kwa tume hiyo, inayobainisha uhalali wa watu hao kuwa wabunge.
Wanachama hao waliokuwa wabunge wa viti maalumu, baada ya kuvuliwa uanachama wao Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kutokana na ukosefu wa nidhamu, walikosa sifa za kuendelea kuwa wabunge.
Wanachama hao ni Saumu Heri Sakala, Salma Mohamed Mwassa, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari Haji, Khadija Salum Ally Al-Qassmy na Halima Ali Mohamed. Baada ya kuvuliwa uanachama na kuvuliwa ubunge, NEC ilitangaza majina ya wabunge wapya waliochukua nafasi za wabunge, ambao tayari waliapishwa na wanaendelea kulitumikia Bunge hilo.
CHANZO HABARI LEO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa