Home » » KITUO CHA DALADALA JAMATINI KUENDELEA KUTUMIKA, MABASI YA MIKOANI YAONYWA

KITUO CHA DALADALA JAMATINI KUENDELEA KUTUMIKA, MABASI YA MIKOANI YAONYWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi akifafanua jambo wakati Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge alipozungumza na wadau wa usafishaji katika Stendi Kuu ya muda ya Mabasi ya Mikoani iliyopo eneo la Nanenane jana Aprili 3, 2018 alipofanya ziara fupi katika stendi hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge akizungumza na wadau wa usafishaji katika Stendi Kuu ya muda Mabasi ya Mikoani iliyopo eneo la Nanenane jana Aprili 3, 2018 alipofanya ziara fupi katika stendi hiyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (katikati) akifafanua jambo wakati Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge (kushoto) alipofanya ziara fupi kukagua maeneo yanayoweza kuwekewa miundombinu muhimu na kutumika kama kituo cha daladala cha Mjini, jana Aprili 3, 2018. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Idara ya Ujenzi Mhandisi Ludigija Ndwata. 


Na Ramadhani Juma,Ofisi ya Mkurugenzi

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge ameelekeza matumizi ya kilichokuwa kituo Kikuu cha Mabasi madogo maarufu kama Daladala cha Jamatini Mjini Dodoma kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria wanaotoka katika maeneo mbalimbali ya Manispaa hiyo yaendelee kama kawaida wakati Manispaa ikiandaa eneo mbadala.

Mkuu huyo wa Mkoa pia ameagiza ‘ruti’ za Daladala zifupishwe kama ilivyokuwa awali, na kwamba upangaji wa ‘ruti’ ndefu ujadiliwe upya na wadau wote wanaohusika na endapo utakubaliwa na wengi ndipo utekelezaji wake uanze.

Dokta Mahenge ametoa maelekezo hayo leo Aprili 3, 2018, alipokuwa akizungumza na wadau wa usafirishaji katika kituo kikuu cha mabasi ya Mikoani cha muda kilichopo Nanenane Manispaa ya Dodoma baada ya kituo hicho kufungwa wiki iliyopita kwa ajili ya kupisha mradi wa Reli ya Kisasa.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya majadiliano na wadau wote ikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMTRA), Manispaa, Jeshi la Polisi, na Shirika la Reli ambao ndio wamiliki wa eneo hilo, na kwamba matumizi ya stendi hiyo yataendelea kwa muda wa miezi miwili kuanzia sasa, kipindi ambacho Manispaa itatakiwa kuwa imeshapata na kuandaa stendi mbadala.

Akizungumza katika eneo la tukio, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi alisema Manispaa imepokea maagizo yote na itahakikisha inaandaa eneo kwa ajili ya Stendi ya Mabasi madogo Mjini katika kipindi cha miezi miwili kama ilivyoelekezwa na Mkuu wa Mkoa.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa ameagiza mabasi yote yanayosafirisha abiria Mikoa mbalimbali Nchini kupakia na kuanzia safari zao katika kituo Kikuu cha mabasi ya muda kilichopo Nanenane na Kampuni itakayokiuka itachukuliwa hatua kali za Kisheria.

“Namuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani wa Mkoa kuwa, kuanzia kesho mabasi yote yauze tiketi na kuanza safari zao hapa katika kituo hiki Kikuu cha mabasi cha muda cha Nanenane…hakuna Mkubwa wala mdogo katika kutoa huduma kwa Wananchi” alisisitiza Dkt. Mahenge.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa