Home » » Rwanda yaruhusu malori ya Tanzania

Rwanda yaruhusu malori ya Tanzania



Dodoma
SERIKALI ya Rwanda imekubali kuruhusu malori ya mizigo katika mpaka wa Tanzania na Rwanda, yaliyokwama kutokana na kupandishwa kwa kodi kutoka dola za Marekani 152 (sh. 243,200) hadi dola 500 (sh. 800,000).
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba, alisema baada ya kutokea kwa hali hiyo, Tanzania iliwasiliana na Serikali ya Rwanda ambayo baada ya muda ilikubali kuyaruhusu malori hayo ya mizigo kutoka Tanzania kuingia nchini humo kwa malipo ya kodi ya zamani.

“Kwanza nikiri kuwa Serikali ilipata taarifa hii juzi kuhusu uamuzi wa Rwanda kupandisha tozo ya malipo, kwa magari ya mizigo kutoka Tanzania.

“Niliwasiliana na Waziri wa Usafirishaji wa Rwanda, Profesa Silas Lwakabamba na kudai hakuna taarifa kama hiyo na baada ya dakika ishirini alinipigia na kunipa jibu la ukweli wa jambo hilo,” alisema Dk. Tizeba.

Alisema Waziri huyo alikiri juu ya jambo hilo, lakini akadai kuwa agizo hilo lilitolewa kwa njia ya mdomo na Waziri wa Fedha na Mipango ya Uchumi, Claver Gatete kuhusu kupandishwa kwa tozo la magari ya mizigo kutoka Tanzania.

Alisema baada ya muda Waziri huyo, alilifanyia kazi suala hilo na malori kutoka Tanzania yakaanza kuingia nchini humo.

“Hivi sasa hakuna tatizo, magari yote yamesharuhusiwa na wafanyabiashara wasiwe na wasiwasi kuhusiana na suala hilo, kwa kuwa tayari limeshapatiwa ufumbuzi na Serikali yao bado inaendelea kuchukua hatua madhubuti katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa jambo hili,” alisema.

Hata hivyo, ilielezwa kuwa hali hiyo inawezekana kwa namna moja au nyingine, ikawa imetokana na mzozo uliopo kati ya Rais Jakaya Kikwete na Rais Paul Kagame wa Rwanda, ambao umesababisha wafanyabiashara wa Rwanda na Uganda kutishia kuacha kupitisha mizigo yao katika Bandari ya Dar es Salaam.

Tanzania na Rwanda zimekuwa katika vita ya maneno, baada ya Rais Kikwete kumshauri Rais Kagame akubali kukutana na waasi wa FDRL, wanaoendelea na vita mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), lakini ushauri huo ulionekana kupokelewa tofauti na Rais Kagame.

Hata hivyo siri ya kupandishwa kwa gharama hizo, zilifichuka juzi baada ya malori mengi ya wafanyabiashara wa Tanzania kukwama katika mpaka wa Rusumo mkoani Kagera.
Chanzo: Tanzania Daima


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa