Home » » KONDOA MJI WAISHUKURU SERIKALI KULETA CHEREHANI 100 KUPITIA UNICEF

KONDOA MJI WAISHUKURU SERIKALI KULETA CHEREHANI 100 KUPITIA UNICEF

Afisa Elimu Awali na Msingi katika Hamashauri ya Mji Kondoa Mwalimu Hassan Mtamba ameishukuru Serikali kupitia shirika la Watoto duniani (UNICEF) ambao ni wafadhili wa program ya Elimu changamani kwa vijana (IPOSA) kwa kuleta chereheni 100 kwa ajili ya kuzigawanya katika vituo 5 ambavyo vinatekeleza program hiyo.

Akiongea baada ya mapokezi ya vifaa hivyo Mwalimu Mtamba amesema cherehani hizo zimekuja na matanki 8 ya maji ya ujazo wa lita 200 kila moja yatasambazwa katika vituo viwili ambavyo vipo katika Shule ya Msingi Kolowasi na King’ang’a ikiwa ni vifaa vya wamu ya pili ambapo awali wamepokea vifaa vya ufundi seremala.

Akiongea kwa upande wake Mwalimu Ashura Mwaya mratibu wa Program ya IPOSA amesema mpango huu ulianzishwa na serikali kwa ajili ya kuwasaidia vijana wa kike na kiume walio nje ya mfumo rasmi wa shule ili waweze kupata ujuzi mbalimbali utakaowasaidia kujipatia kipato kwa kujiajiri au kuajiriwa.

“Katika Halmashauri ya Mji Kondoa vituo vipo katika Shule ya Msingi Maji ya Shamba, Shule ya Msingi Kondoa, Shule ya Msingi King’ang’a, Shule ya Msingi Chandimo na Shule ya Msingi Kolowasi ambapo jumla wapo wanafunzi 449 ambao wanaendelea na mafunzo ya fani mbalimbali yanayotolewa,”amesema Mwalimu Ashura

Ameongeza kuwa vijana wenye umri wa miaka 14 hadi 22 ndio wanaoruhusiwa kujiunga katika mpango huo ili waweze kupata ujuzi wa ufundi seremala, ushonaji, uchomeleaji, mapishi na ujasiriamali kama kutengeneza sabuni na karanga ambavyo wanaweza kuviuza na kujipatia kipato kitakachowasaidia wao na taifa kwa ujumla.

Aidha amesema kuwa mafunzo hayo yanatolewa katika vituo hivyo bila malipo yoyote kwani serikali imegharamia vifaa na kuwalipa walimu na wanafunzi wanajiunga muda wowote hakuna muda maalum wa kujiunga ili kupata vijana wengi ambao wapo nje ya mfumo rasmi.

Programu ya IPOSA ilianza mwaka 2019 katika Halmashauri ya Mji Kondoa ambapo vituo vitano vilichaguliwa na vina jumla ya wanafunzi 449 ambao wapo nje ya mfumo rasmi wa elimu kutokana na changamoto mbalimbali kama kuacha shule au kushindwa kuendelea na masomo baada ya kumaliza elimu ya msingi.


 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa