#Barabara za zege zaonesha ufanisi, zafungua maendeleo
#TAMISEMI kuhakikisha mlima huo unaboreshwa na kupitika muda wote
Na. Catherine Sungura, Kibakwe - Mpwapwa
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
na Mbunge wa Kibakwe, Mhe. George Simbachawene ameishukuru na
kuipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kuanza
kujenga barabara za zege kwenye milima mikali iliyopo kata ya
Mang’aliza-Kibakwe wilayani Mpwapwa.
Waziri
Simbachawene ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya
ujenzi wa miundombinu inayosimamiwa na TARURA iliyofanywa na Naibu
Katibu Mkuu wa OR-TAMISEMI anayeshughulikia miundombinu Mhandisi
Rogatus Mativila .
“Niwashukuru sana TARURA na
kuwapongeza kwa kutusaidia tulio kwenye mazingira magumu, jimbo langu la
Kibakwe lipo katika maeneo tambarare na milimani, na hii ni milima
mikali ambayo ipo karibu kata sita na hakuna namna yoyote ya kutengeneza
barabara zaidi ya barabara za zege”.
Ameongeza
kusema kuwa utaratibu huo wa TARURA wa kujenga barabara za zege
waliouanza miaka michache iliyopita umeanza kuleta ufanisi mkubwa
hususani kufungua maendeleo pamoja na kuwaletea huduma nyingine wananchi
ikiwemo umeme, shule ya sekondari pamoja na kituo cha afya.
“Kata
ya Mang’aliza haikuwa na maendeleo kabisa lakini hii barabara
ilivyofunguliwa hivi karibuni imeleta maendeleo kwa wananchi kwani miaka
ya nyuma nilikuwa nakuja huku kwa pikipiki lakini sasa hivi nakuja kwa
gari na hata magari makubwa yanafika kuleta vifaa vya ujenzi ambapo
kuna shule ya sekondari inajengwa, kwasababu sehemu korofi zote wameweka
zege, kwakweli nawapongeza TARURA”, aliongeza Mhe. Simbachawene.
“Hata
hivyo ombi langu tu waendelee kutenga fedha kwa maeneo mengine kwani
Ilani na sera yetu sasa ni kuwapelekea umeme na huduma nyingine
wananchi lakini changamoto ilikuwa ni barabara ila kusema ukweli TARURA
wamejitahidi sana kwani fedha zinazohitajika ni nyingi ila kwa hicho
kidogo wamefungua hizo barabara na sasa zinapitika na shughuli za
kijamii zinaendelea kama kawaida" alisisitiza.
Aidha,
Mhe. Simbachawene aliwapongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa kuhangaika kutafuta rasilimali fedha, watendaji wa TARURA kwa kazi
nzuri pamoja na TAMISEMI kwa usimamizi ambapo ana imani nia ya kufungua
barabara zaidi itaendelea.
Naye, Naibu Katibu
Mkuu OR-TAMISEMI Mhandisi Rogatus Mativila amesema mlima huo wenye urefu
wa Km. 5 umekuwa mgumu sana kupitika wakati wa kiangazi na hata masika
ambapo chini ya mlima huo kuna uzalishaji mkubwa kutoka kwa wafugaji na
wakulima wa mazoa mbalimbali ambapo TARURA wameweza kutengeneza maeneo
korofi kwa kujenga barabara za zege la saruji lililochanganywa na
kototo pamoja na nondo ambapo hivi sasa barabara hiyo inapitika.
Mhandisi
Mativila amesema kwamba wao kama OR-TAMISEMI wataendelea kuhakikisha
mlima huo unaboreshwa na kupitika muda wote na kuahidi kuendelea kutoa
fedha zaidi ili wananchi waendelee kuzalisha mazao mbalimbali na
kupatiwa huduma za kijamii ikiwemo shule na afya.
0 comments:
Post a Comment