Home » » PROFESA SOSPETER MUHONGO KIKAANGONI LEO

PROFESA SOSPETER MUHONGO KIKAANGONI LEO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Profesa Sospeter Muhongo.
 
Bunge leo linatarajiwa kulipuka kutokana na mjadala mkali unaotarajiwa kutawala wakati wa kujadili hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini iliyowasilishwa bungeni jana jioni na waziri mwenye dhamana, Profesa Sospeter Muhongo.
Hotuba ya Waziri Muhongo inaonekana kuvuta hisia si za wabunge peke yake, bali pia hata wananchi kutokana na unyeti wa wizara hiyo inayokabiliwa na changamoto lukuki katika sekta zake zote muhimu kama umeme, gesi, madini na mafuta.

Awali, makadirio ya bajeti ya wizara hiyo yalizuiwa kuwasilishwa bungeni na Kamati ya Bunge ya Bajeti chini ya uenyekiti wake, Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.

Taarifa ambazo NIPASHE ilizipata zilieleza kuwa kuzuiwa kwa bajeti ya wizara hiyo kuwasilishwa bungeni, kulitokana na serikali kutoipatia wizara hiyo takriban Sh. bilioni 104 zilizotarajiwa kupatikana kutokana na tozo la kodi la Sh. 50 kwa kila lita moja ya mafuta ya dizeli na petroli kwa mwaka wa fedha wa 2013/14.

Fedha hizo zililenga kusaidia usambazaji wa umeme maeneo ya vijijini.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, aliliambia NIPASHE kuwa serikali imeipatia wizara hiyo Sh. bilioni 79 kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini (Rea) huku ikiahidi kuwa kiasi kilichosalia kinatarajiwa kutolewa kabla ya mwisho wa Juni, mwaka huu.

Kwa mujibu wa habari hizo, Kamati ya Bunge ya Bajeti, iliishauri serikali kuahirisha kuwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa kuwa wabunge wengi wangehoji fedha hizo za Rea kama wizara ilikabidhiwa.

Kwa msingi huo, Kamati ya Bunge ya Bajeti iliiagiza serikali kuhakikisha kwamba fedha hizo zinapatikana na kupelekwa kwa wizara hiyo hiyo kwa ajili ya miradi ya umeme vijijini ndipo bajeti ya wizara hiyo iwasilishwe bungeni.

Suala la kukatikakatika kwa umeme mara kwa mara na kutokuwa na umeme wa uhakika katika maeneo kadhaa ya nchi hususan vijijini, ni jambo ambalo dhahiri wabunge wengi watalipigia kelele, hali itakayomfanya waziri mwenye dhamana kuwa na wakati mgumu kutoa majibu ya kuwaridhisha.

GESI
Aidha, kwa upande wa gesi, Waziri Muhongo amekuwa akiponda uwekezaji wa wazawa katika sekta ya gesi kwa maelezo kwamba unahitaji mtaji mkubwa.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Waziri Muhongo, imekuwa ikipingwa na wadau wengi wakisisitiza kuwa ni muhimu wananchi wapewe kipaumbele katika uwekezaji wa rasilimali yao kabla ya wawekezaji wa kutoka nje.

Hali hiyo ndiyo inayoashiria kuwa ndani ya Bunge leo kutawaka moto na Waziri Muhongo atabanwa kwa mambo hayo na mengine mengi ili atoe ufafanuzi.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa