TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Ziara ya Mhe. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa
Morocco nchini 12 -13 Julai, 2017
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Serikali
ya Ufalme wa Morocco Mhe.Mounia Boucetta
na ujumbe wake wametembelea Wizara leo tarehe 13 Julai, 2017 na kufanya
mazungumzo na mwenyeji wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Suzan Kolimba katika ukumbi wa Wizara, Dar es
Salaam. Mhe. Mounia Boucetta yupo nchini kwa ziara ya kikazi tangu tarehe 12
Julai, 2017.
Lengo la ziara hiyo ni kufuatilia utekelezaji wa Maazimio na makubaliano
ya Ushirikiano kati ya taasisi za Tanzania na Morocco katika sekta mbalimbali,
yaliyosainiwa wakati wa ziara ya Mfalme Mohammed VI wa Morocco nchini Tanzania
tarehe 23 – 25 Octoba, 2016.
Itakumbukwa katika ziara hii jumla ya mikataba 21 ya Ushirikiano katika
maeneo mbalimbali ilisainiwa. Mikataba hiyo ni katika masuala yafuatayo; Masuala ya Usafiri wa Anga, Kilimo na Uvuvi, Nishati,
Utalii, Viwanda Usafiri wa Reli, Biashara, Masuala ya Bima, Masuala ya Afya,
Masuala ya Gesi, Masuala ya Siasa, Uchumi, Sayansi na Utamaduni.
Aidha Mheshimiwa Mfalme Mohamed VI aliahidi mambo makuu matatu
·
Ujenzi wa
msikiti mkubwa wa kisasa jijini Dar es salaam
·
Ujenzi wa
uwanja wa kisasa wa mpira mjini Dodoma
·
Kuanzisha
programu ya mafunzo kwa maafisa wa majeshi yetu ya ulinzi na usalama
Tangu ziara hiyo ifanyike Serikali ya Ufalme wa Morocco, katika
kuimarisha urafiki na ushirikiano ilifungua Ubalozi wake jijini Dar es
salaam, na Mwezi Februari, 2017 Mheshimiwa Balozi Abdelillah Benryane
aliwasilisha hati zake za utambulisho Nchini.
Wizara inawataarifu kuwa Ubalozi umeanza kufanya kazi nzuri, kazi
mojawapo kubwa ni kufuatilia utekelezaji wa mikataba hiyo iliyosainiwa wakati
wa ziara ya Mheshimiwa Mfalme.
Hivyo ujio wa Mheshimiwa Naibu Waziri Mounia Boucetta ni sehemu ya
ufuatiliaji wa hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mikataba hiyo
iliyosainiwa.
Wizara ilifanya kikao na Mheshimwa Mounia Boucetta na kupitia taarifa ya utekelezaji wa mikataba
hiyo kwa sekta ya umma na sekta binafsi, na kwa kweli tunaridhishwa na kasi ya
utekelezaji.
Pamoja na kasi nzuri hiyo ya utekelezaji Wizara imezielekeza taasisi
husika kuongeza kasi zaidi ili tukamilishe utekelezaji wa maeneo hayo
tuliokubaliana na kuwawezesha Watanzania wafanyabiashara, wakulima, wazalishaji
na wasomi kunufaika na fursa mbalimbali.
Aidha, akizungumza katika majadiliano hayo Naibu Waziri Mhe. Dr. Suzan
Kolimba (Mb) amesema wamekubaliana kuundwa Kamati ya Ufuatiliaji ya utekelezaji
wa makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa kati ya Tanzania na Morocco.
Mhe. Mounia Boucetta pamoja na ujumbe wake leo saa 4:00 asubuhi
watakutana na ujumbe wa wadau wa biashara na uwekezaji kutoka Wizara na taasisi
za Serikali pamoja na taasisi binafsi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika
Hoteli ya Serena, Dar es Salaam
-Mwisho-
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es
Salaam, 13 Julai, 2017
|
0 comments:
Post a Comment