SERIKALI imetoa siku saba kwa halmashauri ambazo hazijamaliza
matumizi ya fedha hasa kwa upande wa ununuzi wa dawa na vifaa tiba kutoa
maelezo kwa njia ya maandishi ni kwanini fedha hizo hazijatumika kama
zilivyopangwa wakati wananchi wakilalamika kukosa dawa na kwanini
wasichukuliwe hatua.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), George Simbachawene alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati
akizungumza kwenye mkutano wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya
uliomalizika mjini hapa. Agizo hili linawahusu Makatibu Tawala wa Wilaya
na Mikoa yote hapa nchini.
Alisema hali ya matumizi ya fedha katika halmashauri nyingi ni
changamoto kubwa kwani licha ya wananchi kukosa dawa na vifaa tiba bado
kuna halmashauri zina fedha nyingi kwenye akaunti zao na kuvuka mwaka wa
fedha na wakiwa na bakaa. Waziri huyo alisema si lengo la serikali
kuwepo na fedha zinazovuka mwaka, hasa ikizingatiwa kuwa katika mwaka wa
fedha 2016/17 fedha za mfuko wa pamoja wa Afya (HBF) zilifika kwenye
mikoa na halmashauri kwa wakati lakini bado wananchi hawana dawa na
vifaa tiba.
Aliwaagiza makatibu tawala wa mikoa yote 26 kwamba halmashauri zote
ambazo hazijamaliza matumizi ya fedha hasa upande wa ununuzi wa dawa na
vifaa tiba zitoe maelezo. “Nawapa wiki moja kuanzia leo zilete maelezo
kwa maandishi ni kwanini fedha hizo hazijatumika kama zilivyopangwa
ilihali wananchi wanalalamika kukosa dawa na ni kwa sababu zipi
wasichukuliwe hatua,” alisema Waziri Simbachawene.
Alisema mwaka 2015/16 fedha hizo zilitolewa bila kujali matokeo kwa
nia ya kuzitaka halmashauri kutumia fedha hizo kuboresha huduma kabla
hazijaanza kupimwa kwa matokeo, isipokuwa fedha za mkopo kutoka Benki ya
Dunia zilitolewa kwa njia ya matokeo kwa kutumia utaratibu huo. “Si
halmashauri zote zilifanikiwa kupata fedha hizo, makatibu tawala wa
mikoa wanatakiwa kuhakikisha halmashauri zinafikia vigezo vilivyowekwa
ili kusitokee tena halmashauri kupoteza fedha hizo,” alisema.
Hata hivyo, alisema serikali kwa kushirikiana na wadau, wameamua
kuanzia mwaka huu wa fedha 2017/18, serikali itaanza kupeleka moja kwa
moja kwenye akaunti za vituo vya kutolea huduma za afya ikiwa ni katika
hatua ya kuimarisha huduma za afya ngazi za msingi na kudhibiti upotevu
na uchelewaji wa fedha kuwafikia watoa huduma.
Alisema katika kufanya kwa vitendo falsafa ya Tamisemi mpya imekuja
na utaratibu wa kuwa na mkataba wa ufanisi wa kazi kwa viongozi.
“Sitasikia halmashauri imevuka mwaka huu tulioumaliza na mabilioni ya
fedha kuingia mwaka 2017/18, sitasikia malalamiko yanayohusu lugha chafu
na isiyo na staha kwa wateja na dawa muhimu zinapatikana kwa wakati
wote. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wadau wa maendeleo, kutoka Ubalozi
wa Uswis, Thomas Teuscher alisema sekta ya afya nchini inakabiliwa na
changamoto nyingi na serikali ijitahidi kufanya maboresho ili kuboresha
huduma za afya kwa ujumla hasa katika suala la uwajibikaji.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment