Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Viongozi
wa Dini Watangaza Siku Saba za Kumwombea Rais Magufuli
Na
Jonas Kamaleki- MAELEZO
Viongozi wa dini wametangaza maombi ya siku saba nchi nzima kumwombea Rais John
Pombe Magufuli ili aendelee na juhudi zake za kulinda raslimali za watanzania
kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam katika
mahojiano maalum na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki
za Binadamu kwa jamii ya dini zote, Askofu William Mwamalanga kwa niaba ya
viongozi wa dini.
“Tumeamua kufanya maombi ya siku saba kwa kumtaka
kila mtanzania popote alipo kutembea hatua saba kila siku akimwombea Mhe. Rais
Magufuli ili Mungu amlinde pamoja na anaofanyanao kazi kwa usahihi (uaminifu)”,
alisema Askofu Mwamalanga.
Ndani ya siku hizo saba kila mtanzania atakuwa
ametembea jumla ya hatua 49 akimwombea Rais Magufuli na wezalendo wenzake.
Kwa mujibu wa Kiongozi huyo wa Dini, maombi hayo
yataanza kesho Alhamisi Juni 15(leo) nchi nzima na yatajumuisha watu wa dini
zote nchini, yaani madhehebu ya Kiislam, Kikristo, Kihindu, Budha na madhehebu
mengine.
Maombi haya yanafanyika baada ya kuona kuwa Mhe.
Rais Magufuli kuchukua hatua madhubuti za kutaka waliohusika kwa namna yoyote
kuiba raslimali za Taifa hususani madini, wanachukuliwa hatua na kuitaka
kampuni ya ACCASIA kulipa kile ambacho walichukua kinyume cha sheria.
Askofu Mwamalanga amesema kuwa Kamati yake
inamwomba Rais Magufuli achukue hatua za haraka kudhibiti raslimali za nchi kwa
upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambako mali nyingi zinatoroshwa na
wajanja wachache.
Kamati hiyo ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki
za Binadamu kwa jamii ya dini zote imemwomba Mhe. Rais aziunganishe Wizara za
Nishati na Madini na Maliasili na Utalii na kuunda wizara moja ambayo
itasimamia kwa karibu raslimali za watanzania.
“Tunamwomba Rais Magufuli amchague mtu makini na
mzalendo mwenye uchungu na nchi hii ili asimamie wizara hiyo, na nina hakika
wizara hiyo ikisimamiwa vizuri, ndoto ya Rais ya kuifanya Tanzania kuwa nchi
mhisani itatimia kwa kuwa hapa Mungu ametujalia kila kitu”,alisema Askofu
Mwamalanga.
Viongozi hao wamempongeza Rais Magufuli kwa
Uzalendo na Ujasri alionao katika kulinda raslimali za Taifa na kupambana na
maovu. Wamesema ni kiongozi wa kuigwa na Marais au viongozi Duniani kote.
Kuhusu suala la walioachishwa kazi kutokana na
kuwa na vyeti feki, Askofu Mwamalanga amesema kuwa Kamati inamwomba Mhe Rais
kuwasamehe wale ambao wameitumikia nchi hii kati ya miaka mitano na 30 ili
walau wapatiwe kifuta jasho licha ya kwamba walitumika bila kuwa na vyeti halali
vya Kidato cha nne.
“Msamaha tunaoomba si wa kuwarudisha kazini bali
tunaomba kwa ajili ya kupata kiinua mgongo kwani wengine walitumika kwa
uaminifu na hata kupewa tuzo za ufanyakazi hodari (bora) hasa katika sekta za
Afya,wauguzi, Elimu na maeneo mengine”, alisema Askofu Mwamalanga.
Mapema wiki hii, Rais Magufuli alipokea ripoti ya
pili ya uchunguzi wa makinikia ambayo iliwajumuisha wanasheria na wachumi.
Katika ripoti hiyo ilibainika kuwa kiasi kikubwa cha madini kilichukuliwa bila
watanzania kupata chochote. Takriban madini yenye thamani ya shilingi trilioni
108 yalisafirishwa nje ya nchi bila Tanzania kupata faida kutokana na madini
hayo.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment